Thursday, 23 April 2015

Yanga kuzidi kuukaribia ubingwa leo

*Wanarudiana na Maafande wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa

Na Mwandishi Wetu
VIONGOZI wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga (pichani), leo wanashuka katika dimba la taifa jijini Dar es Salaam kucheza na maafande wa Ruvu Shooting katika mchezo muhimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga wanashuka uwanjani huku wakiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare na maafande hao katika mchezo wa raundi ya kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye uwanja huohuo.

Vijana hao wa kocha Hans van der Pluim wameshinda mechi sita mfululizo huku leo kikosi cha Mkenya Tom Olaba kitakuwa na kibarua cha kuwalinda vikali washambuliaji wenye uchu wa mabao wa Yanga.

Baadhi ya washambuliaji wake hao ni Simon Msuva, Amissi
Tambwe, Kpah Sherman na Mrisho Ngassa, ambao wamekuwa wakifunga mabao kama hawana akili nzuri na kuiwezesha Yanga kucheza mechi zao za mwisho mwisho kwa kishindo.

Timu hiyo yenye pointi 49 kileleni, inahitaji pointi sita tu ili kuivua ubigwa Azam FC, huku ikisubiri kucheza Polisi Morogoro Jumatatu, Azam FC itacheza nao Mei 6 kabla ya kuhitimisha kwa kucheza na Ndanda FC ugenini Mei 9.

Yanga wanatofautiana na Ruvu Shooting kwa pointi 20 ikiwa na maana kuwa vijana hao wa Jangwani hadi sasa wamejikusanyia jumla ya pointi 49 wakati wapinzani wao hao wa leo wana pointi 29 tu.

Hakuna ubishi kuwa maafande hao wamekuwa hawana matokeo mazuri katika baadhi ya mechi zao zilizopita, baada ya kufungwa na Kagera Sugar 2-0 kabla ya kuja kuifunga Mgambo Shooting 2-1 katika mchezo uliopita.

Timu zote mbili zitakumbuka kuwa zilichezeana rafu mchezo wa kwanza, kiasi cha kusababisha baadhi ya wachezaji kupigwa faini kwa utovu wa nidhamu.No comments:

Post a Comment