Thursday, 16 April 2015

Chelsea mbioni kumpiga bei Mbrazil OscarLONDON, England
HATIMAYE kocha wa Chelsea Jose Mourinho anataka kumtema Oscar katika kikosi chake katika kipindi kinachokuja cha majira ya joto huku timu hiyo ikimuwinda mshambuliaji wa West Ham, Enner Valencia.

Oscar ambaye ni kiungo mshambuliaji, alinunuliwa na klabu hiyo kwa ada ya uhamisho ya kitita cha pauni Milioni 25 katika kipindi cha majira ya joto cha mwaka 2012 wakati Roberto di Matteo akiwa kocha wa timu hiyo.

Mchezaji huyo alitokea katika timu ya kwao Brazil ya Internacional, ambako alionesha kiwango cha hali ya juu.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 ni miongoni mwa mahiri katika Ligi Kuu ya England msimu huu, lakini ameshindwa kuendana na mfumo wa Mourinho.

Oscar hajaanza au kumaliza dakika zote 90 katika mashindano yoyote tangu januari mwaka huu.

Mabingwa wa Italia Juventus wana nia ya kumchukua mchezaji huyo, huku Valencia akitajwa na the Blues baada ya kuonesha kiwango cha hali ya juu West Ham tangu alipowasili kwa ada ya pauni Milioni 12m akitokea timu ya Mexico ya Pachuca Julai mwaka jana.


Hatahivyo, West Ham tayari imesisitiza kuwa itafanya kila iwezalo kuhakikisha mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ambaye anaichezea timu ya taifa ya Ecuador anabaki katika klabu hiyo.

No comments:

Post a Comment