Friday 3 April 2015

Mashabiki Simba wafa ajalini wakienda Shinyanga kushangilia timu



 *Leo Jumamosi wanacheza na Kagera Sugar ya Bukoba

Na Mwandishi Wetu
WAKATI timu ya Simba leo inashuka dimbani kucheza na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, mashabiki wake saba wamekufa katika ajali ya gari mjini Morogoro wakiwa njiani kwenda kuishangilia timu hiyo itakayocheza leo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa jana usiku na kituo cha televisheni cha Star, mashabiki hao walipata ajali sehemu moja mkoani Morogoro wakienda Shinyanga kuishangilia timu yao.

Saba kati yao walifariki dunia na wengine kujeruhiwa. Hatahivyo, taarifa hiyo haikuwa na maelezo zaidi na kituo hicho kilisema kitaendelea kutoa taarifa zaidi za ajali hiyo kila watakapopata taarifa.

Aidha, Simba inashuka dimba leo ikitaka kulipa kisasi cha cha kufungwa na Kagera Sugar katika mechi ya mzunguko wa
kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Timu hiyo yenye maskani yake barabara ya Msimbazi jijini Dar es Salaam, ilikubali kichapo cha bao 1-0 kwenye uwanja wake wa Taifa kwa bao lililowekwa kimiani na Atupele Green mwishoni mwa mwaka jana.

Simba pia imepania kushinda katika mchezo wa leo baada
ya kushinda mchezo wao wa mwisho wa ligi dhidi ya Ruvu
Shooting 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, kabla ya mapumziko ya ligi hiyo kupisha mechi za kimataifa za kalenda ya Fifa.

Kagera Sugar imekuwa ikitumia uwanja huo wa Kambarage kama  uwanja wa nyumbani baada ya ule wa Kaitaba mjini
Bukoba kufungwa ukifanyiwa matengenezo.

Nayo Kagera iko katika ari kubwa baada ya kuibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya ndugu zao wa Mtibwa Sugar kwenye uwanja huohuo Jumatano ya wiki hii.

Timu hizo zinacheza huku zikiwa zimetofautiana kwa pointi
nne, ambapo Simba iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 32 wenzao wa Kagera Sugar wana pointi 28 baada ya kila moja kucheza mechi 20.

Msemaji wa Simba, Haji Manara alisema timu yao
imedhamiria kushinda katika michezo yote sita iliyobaki ili kugombania nafasi mbili za juu na kuweza kupata nafasi ya kuliwakilisha taifa kimataifa baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa misimu mitatu sasa.

Naye kocha msaidizi wa Kagera Sugar, Mrage Kabange alisema
wataendeleza kipigo kwa wapinzani hao kwa kuutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani.

Mechi nyingine Jumamosi leo ni kati ya Coastal Union ya Tanga itakayoikaribisha Tanzania Prisons iliyopo mkiani mwa ligi hiyo.

Kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Ndanda FC itakuwa mwenyeji wa Mbeya City huku Ruvu Shooting wakicheza na JKT Ruvu kwenye uwanja wa mabatini Mlandizi mkoani Pwani.

No comments:

Post a Comment