Tuesday 27 March 2018

Taifa Stars, Congo Kumenyana Leo Uwanja wa Taifa


Na Mwandishi Wetu
TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars leo inatarajia kushuka kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya DR Congo.

Stars inacheza na Congo ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 4-1 ilichopata toka kwa Algeria wiki iliyopita katika mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kocha msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Morocco alisema wamejiandaa vema kwa mchezo huo baada ya kupoteza dhidi ya Algeria pamoja na kwamba ana majeruhi wawili.

"Tumejiandaa vizuri kwani ninajua Congo ni timu nzuri na sisi tunahitaji ushindi baada ya kupoteza mchezo uliopita. Kikosi changu kina majeruhi Aishi Manula ambaye anasumbuliwa na kifundo cha mguu na Abdulaziz Makame," alisema Morocco.

Naye nahodha msaidizi wa Stars, Himid Mao alisema wao wamejiandaa kuhakikisha wanawapa raha mashabiki kwani makosa yaliyojitokeza katika mchezo uliopita wameyafanyia kazi.

Kwa upande wa Kocha wa DR Congo, Ibenge Florent alisema anaamini mchezo utakuwa mgumu kwani Taifa Stars itakuwa inapambana kuhakikisha inashinda mbele ya mashabiki wake huku akimtaja Simon Msuva na Mbwana Samatta kama wachezaji wanaowahofia.

"Tanzania ni jirani zetu pia ni ndugu zetu ndiyo maana tumekubali kucheza nao. Mchezo utakuwa mgumu kwani Taifa Stars haitakubali kufungwa kirahisi mbele ya mashabiki wake na wachezaji Samatta na Msuva tunajua wakipata nafasi wanaweza kufunga bao," alisema Ibenge.

Mchezo huo unatarajiwa kuanza saa 10:00 jioni na viingilio ni Sh 5,000 VIP A na B, huku maeneo mengine ikiwa ni Sh 1,000.

No comments:

Post a Comment