Sunday 25 March 2018

Mamlaka Hifadhi ya Ngorongoro Yadhamini Mbio


Na Mwandishi Wetu, Karatu
MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) itadhamini Ngorongoro Marathon 2018 zitakazofanyika Aprili 21 kwa Sh milioni 30.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Karatu, Arusha Mkurugenzi wa mbio hizo, Meta Petro alisema jana kuwa mamlaka hiyo imekubali kudhamini mbio hizo zitakazofanyika Aprili 21 mwaka huu.

Petro alisema kuwa NCAA ndio mdhamini mkuu wa mbio hizo, ambazo mwaka huu ni za 11 kufanyika tangu zilipoanzishwa na zimekuwa zikikua mwaka hadi mwaka.

Alisema kuwa anatarajia mbio za mwaka huu kushirikisha wanariadha wengi kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo wakimbiaji mbalimbali nyota.

Mbali na NCAA, wadhamini wengine ni Kampuni ya Vinywaji ya Bonite, ambao wamekubali kuendelea kudhamini mbio hizo kwa kutoa bidhaa mbalimbali zenye thamani ya Sh milioni 15.

Petro alisema kuwa anawashukuru wadhamini hao na bado milango iko wazi kwa wengine kujitokeza kusaidia kudhamini ili kuzidi kufanikisha mbio hizo, ambazo zitaanzia katika lango kuu la kuingilia na kutokea katika Hifadhi ya Ngorongoro na kumalizika katika viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu.



No comments:

Post a Comment