Tuesday 6 March 2018

Simba Uso kwa Uso na Al Masry Uwanja wa Taifa


Na Mwandishi Wetu
SIMBA leo itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiikaribisha timu ya Al Masry ya Misri katika mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika utakaoanza saa 12:00 jioni.

Wawakilishi hao wa Tanzania wanaingia uwanjani wakiwa na ari ya ushindi ili kupunguza kazi katika mchezo wa marudiano, kwani Waarabu wana tabia ya kucheza kwa kujihami ugenini na nyumbani kushambulia sana.

Kocha wa Simba Mfaransa, Pierre Lechantre alisema anaifahamu Al Masry na timu nyingine za Misri kuwa ni timu zinazocheza soka la kujihami zikiwa ugenini, lakini nyumbani wanashambuliaji hivyo watajitahidi kuhakikisha wanapata ushindi nyumbani ili ugenini wawe na kazi nyepesi.

“Wachezaji Emanuel Okwi na John Bocco watakuwepo lakini sisemi tutaingia kwa staili gani bali tutacheza kutafuta ushindi kwa sababu timu zinazotoka nchi za Kiarabu zinatabia ya kucheza mchezo wa kujihami ugenini,” alisema Lechantre.

Naye nahodha wa timu hiyo, John Bocco alisema matokeo ya sare ya 3-3 ya Ligi Kuu dhidi ya Stand United yasiwatie hofu waje kwa wingi kuishangilia timu yao, kwani wachezaji wanajua deni walilonalo kwao.
“Kocha amefanya kazi yake na sisi wachezaji tumejiandaa kuhakikisha tunapata ushindi, kwani ni muda mrefu Simba haijashiriki mashindano ya kimataifa hivyo mashabiki waje kwa wingi kuisangilia timu yao,” alisema Bocco.

Wakati Simba ikiongoza Ligi Kuu Tanzania Bara, wapinzani wao wanashika nafasi ya nne katika ligi nchini Misri.

Kocha wa Al Masry, Hossam Hassan atakuwa na kumbukumbu ya kipigo alichopata toka kwa Simba wakati akichezea Zamaleck mwaka 2003 baada ya kufungwa bao 1-0 Dar es Salaam na ugenini Simba ikafungwa bao 1-0 na kutolewa kwa penalti 3-2 baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 1-1.

Timu hiyo inamtegemea mshambuliaji raia wa Burkinafaso Aristide Bance ambaye amegeuka gumzo hapa nchini na kwenye mitandao ya kijamii.

Simba ilifuzu hatua ya awali kwa kuiondoa Gendermarie ya Djibout kwa mabao 5-0 wakati wapinzani wao Al Masry walifuzu kwa kuishinda Green Buffalo ya Zambia kwa mabao 5-2.
Kiingilio katika mchezo huo VIP A ni Sh 20, 000, VIP B ni Sh 15,000 na mzunguko Sh 5,000.

Baada ya mchezo wa huo wa leo, timu hizo zitarudiana siku 10 baadaye mjini Cairo, Misri na mshindi wa jumla ataingia kwenye mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi kwa kucheza na moja ya timu zilizotolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu zinazoingia hatua ya makundi Kombe la Shirikisho hupewa dola za Marekani 150,000 (zaidi ya Sh milioni 300), ambazo huongezeka kila timu inaposhinda na kusonga mbele.

Bingwa wa Kombe la Shirikisho hupata Dola za Kimarekani 625,000 (zaidi ya Sh bil 1.5), mshindi wa pili wa Kundi hupata dola 239,000.

No comments:

Post a Comment