Sunday 25 March 2018

Wambura Aendelea Kupinga Maamuzi ya TFF


Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) aliyefungiwa maisha na Kamati ya Maadili, Michael Wambura ameibuka na kulaani uteuzi wa Kamati ya Utendaji kumteua Athumani Nyamlani kukaimu nafasi hiyo.

Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo, juzi ilimteua Nyamlani kukaimu nafasi hiyo, huku ikimthibitisha Kidao Wilfred kuwa Katibu Mkuu katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Wambura katika taarifa hiyo kupitia mwanasheria wake, Emmanuel Muga alisema kuwa anapinga uteuzi huo wa Nyamlani kuchukua nafasi yake wakati rufaa yake aliyokata bado haijasikilizwa na kutolewa uamuzi.

Taarifa hiyo ya kurasa moja inaeleza kuwa Kamati ya Utendaji Machi 24, 2018 iliendesha zoezi la uteuzi lisilo halali na kuvunja ibara namba 34 (1) ya Katiba ya TFF, ambayo inaeleza kuwa nguvu ya kumchagua na kumuondoa makamu wa rais ni ya Mkutano Mkuu.

Pia Wambura ameshtushwa na kitendo cha kuwabadilisha baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Rufaa, ambapo uamuzi huo wa Kamati ya Utendaji sio wa haki na unaopigana na ibara ya 34 (2) ya Katiba ya TFF.
 
Ibara hiyo inasomeka: “Chombo hicho huru cha kisheria cha TFF wajumbe wake hawaruhusiwi kuondolewa kabla ya kipindi chao bila ya kuidhinishwa na Mkutano Mkuu.


Nyamlani anachukua nafasi ya Wambura aliyefungiwa maisha na Kamati ya Maadili kutojihusisha na masuala ya mpira, na Kidao alikuwa akikaimu nafasi hiyo takribani miezi nane sasa.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao cha Kamati ya Utendaji, ambacho kilikutana kwenye hoteli ya Sea Scape zinasema, Nyamlani amepata sifa za kukaimu nafasi hiyo kwa sababu kanuni na taratibu za TFF zinatamka kuwa nafasi za kuchaguliwa mjumbe atakaye kaimu awe mjumbe wa Kamati ya Utendaji aliyedumu kwa kipindi kirefu.

“Kanuni zinamtaka mjumbe wa muda mrefu ambaye yupo kwenye Kamati ya Utendaji, na ukiangalia kwa sasa wajumbe ambao wana muda mrefu ni Nyamlani, Ahmed Mgoyi na Khalid wa Tanga ila sasa Nyamlani ndio amewazidi wote, hivyo kamati ilimkaimisha yeye hadi uchaguzi mdogo utakapotangazwa,” kilisema chanzo hicho.
 
Hata hivyo, kazi ya kumwidhinisha Nyamlani kukaimu nafasi hiyo haikuwa rahisi kwani ililazimika kupigwa kura ili kumpitisha, ambapo zile za ndio zilikuwa nyingi, hivyo akapitishwa mpaka pale mkutano mkuu wa TFF utakavyoamua vinginevyo.

Nyamlani ambaye alikuwa makamu wa Rais kipindi cha uongozi wa Leodgar Tenga,  aliingia kwenye Kamati ya Utendaji kwa kuteuliwa na Rais Wallace Karia yeye na Ahmed Mgoyi.

Kidao alikuwa akikaimu nafasi ya ukatibu mkuu baada ya yule wa awali, Selestine Mwesigwa, yeye na Malinzi kushtakiwa kwa madai ya ubadhilifu na makosa mengine.

No comments:

Post a Comment