Monday 19 March 2018

Chuoni Yaitambia Miembeni City kwa Bao 1-0


Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Chuoni, Suleiman Jabir `Mdau' (kulia) akiwa na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi (katikati). Kushoto ni mpenzi wa michezo, Ally Nyonyi.

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

TIMU ya soka ya Chuoni juzi iliitambia Miembeni City kwa kuondoka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Zanzibar Kanda ya Unguja uliochezwa kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.

Mchezo huo uliochezwa majira ya saa 10:00 za jioni ulikuwa na ushindani kiasi huku kila upande yukionekana kutoa malalamiko ya kutotendewa haki na mwamuzi aliechezesha mchezo huo.

Bao hilo la pekee liliwekwa kimiani na mchezaji wake Rashid Roshwa mnamo dakika ya 73 za mchezo huo, ambao kabla ya huo Polisi ilishuka kuumana na Kipanga na kushinda mabao 3-1.

Chuoni licha ya ushindi huo bado ipo katika nafasi ya nne kutoka mkiani ikiwa na pointi 22 katika msimamo wa ligi hiyo inayoongozwa na KVZ wenye pointi 35.

Katika mchezo huo, Miembeni City ilikosa penalti katika dakika ya 85 kupitia kwa mchezaji wake, Yahya Haji Karoa, penalti ambayo ilitokana na Seif Salum kufanyiwa madhambi na mlinda mlango wa timu ya Chuoni.

Mchezo mwingine ambao uliwakutanisha Polisi na Kipanga ambapo Polisi ilitoka na ushindi wa bao 3-1, huku mabao yake yalifungwa na Suleiman Ali Nuhu dakika ya 11 na mawili yalifungw ana Suleiman Mwalimu dakika ya 55 na 78.

Polisi kwa matokeo hayo imefikisha pointi 26 na kuwa nafasi ya nane katika msimamo wa ligi hiyo, wakati Kipanga inabaki katika nafasi ya pili kutoka Mkiani ikiwa na pointi 11.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena kesho kwa  mchezo mmoja ambao utawakutanisha Taifa ya Jang’ombe na Miembeni City.


No comments:

Post a Comment