Wednesday 28 March 2018

Serikali Yaiaga Timu ya Madola, Yachimba Mkwara

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe akimkabidhi bendera ya taifa nahodha wa timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola, Masoud Mtalaso, katika hafla iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Rais wa TOC, Gulam Rashid na kulia ni Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi.

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola imeagwa, huku Serikali ikisisitiza kuwa kuanzia sasa haitaruhusu timu au mchezaji asiyeandaliwa vizuri kwenda kushiriki mashindano ya kimaataifa nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam wakati akiikabidhi bendera ya taifa kwa ajili ya Michezo hiyo Gold Coast, Australia kuanzia Aprili  hadi 15.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe (wa pili kushoto) akiwa na timu ya Tanzania jijini Dar es Salaam jana,  itakayoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola. 

Dk Mwakyembe alisema kuwa ni upotevu wa fedha bure kupeleka lundo la wachezaji ambao hawajaandaliwa vizuri, hivyo kuanzia sasa Serikali kupitia Idaya ya Michezo na Baraza la Michezo watahakikisha wachezaji wanaokwenda nje kushiriki michezo ya mkimataifa, ni wale tu walioandaliwa vizuri na kufikia vigezo vilivyowekwa.
Nahodha wa timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola, Masoud Mtalaso akitoa ahadi yaushindi baada ya kukabidhiwa bendera ya taifa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe (kushoto)
Alisema imekuwa tabia ya baadhi ya vyama au mashirikisho ya michezo nchini kutowaandaa vizuri wachezaji wake,  lakini unapofika wakati wa mashindano ya kimataifa wanawapeleka wachezaji kushiriki wakati hawajawaandaa.

Awali, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema kuwa walitoa mwongozo kwa vyama kuhusu maandalizi ya michezo hiyo, lakini vimeshindwa kabisa kutoa ushirikiana.
Alisema vyama ndivyo vyenye jukumu la kuandaa wachezaji lakini baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa vyama, wamekuwa wakifikiri kuwa jukumu hilo ni la TOC.

Alisema kuwa awali walitakiwa kupeleka wachezaji 34 lakini imebidi wapeleke 16 tu wa michezo ya riadha, ngumi, mpira wa meza pamoja na kuogelea baada ya kushindwa kufikia vigezo vilivyoweka ikiwemo kufuzu.
Alisema kuwa TOC imetumia zaidi ya Sh milioni 180 kwa ajili ya kugharamia kambi ya mwezi mmoja, nauli ya wachezaji, makocha na viongozi wa timu hiyo.
Timu ya taifa ya ndondi itakayoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola 2018
Mwakyembe alikabidhi bendera hiyo kwa nahodha wa timu hiyo inayoondoka leo kwenda Gold Coast, Masoud Mtalaso, ambaye ni mchezaji wa mpira wa meza na aliahidi kufanya vizuri katika michezo hiyo.
Wachezaji wa timu ya taifa ya mpira wa meza wakiwa na nyuso za furaha.

Timu ya taifa ya riadha pamoja na viongozi wao.

Timu ya kuogelea.
Kocha na Matron, Lwiza John.

Meneja wa timu ya Tanzania, Nasra Mohamed.
Kocha Mkuu wa timu ya riadha, Zacharie Barie.


No comments:

Post a Comment