Tuesday 6 March 2018

Yanga Yajiweka Matatani Mabingwa Afrika


Na Mwandishi Wetu
WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika Yanga wamejiweka katika nafasi ngumu ya kufuzu kucheza hatua ya makundi baada ya kufungwa 2-1 na Township Rollers ya Botswana katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 Kwa matokeo hayo, mabingwa hao wa Tanzania Bara, sasa wanahitaji ushindi wa kuanzia angalau mabao 2-0 na kuendelea.

Katika mchezo wa jana wageni waliandika bao la kwanza katika dakika ya 11 kupitia kwa Lemponye Tshireletso aliifungia bao Township bao la kuongoza baada ya kupiga shuti kali nje ya meta 18 lililokwenda moja kwa moja wavuni.

Obrey Chirwa aliisawazishia Yanga katika dakika ya 30 baada ya kupata pasi safi kutoka kwa Tshishimbi.

Yanga walitengeneza nafasi kadhaa za kufunga lakini wachezaji wake hawakuwa makini na  kukosa mabao.

Katika dakika ya tatu, wapinzani wa Yanga nusura wafunge baada ya Joel Morogorosi kutokuwa makini na mpira kuwahiwa na kipa wa Yanga, Ramadhani Kabwili.

Ibrahim Ajib alikosa bao katika dakika ya 25 baada ya kupiga mpira uliopaa juu ya lango la wapinzani wao hao kutoka Botswana.

Yanga ilianza kwa nguvu kipindi cha pili kwa kufanya mashambulizi kadhaa, ambapo katika dakika ya 48 nusura  wapate bao baada ya Gadiel Michael kushindwa kufunga baada ya kupiga shuti kali lililopaa juu ya lango.

Timu hizo zitarudiana mjini Gaborone, Botswana Machi 17 katika mchezo wa utakaoamua timu ipi itinge hatua ya makundi huku Yanga ikiwa na kibarua kigumu zaidi.
Nahodha wa Yanga, Pius Buswita akizungumza baada ya mchezo huo jana alisema kuwa wapinzani wao walitumia vizuri nafasi walizopata, lakini na wao wanaweza kushinda katika mchezo huo wa ugenini.

 Kikosi cha Yanga: Ramadhani Kabwili, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Said Ali, Kelvin Yondan, Papy Tshishimbi, Pius Buswita, Pato Ngonyani, Ibrahim Ajibu/Juma Mahadhi, Obrey Chirwa na Emmanuel Martine/Mwashiuya.

No comments:

Post a Comment