Friday 29 December 2017

Ligi Kuu Bara kuendelea Leo Azam, Stand kuumana

Na Mwandishi Wetu
LIGI Kuu Tanzania Bara (VPL) mzunguko wa 12 msimu wa 2017/2018, inaendelea leo Ijumaa baada ya kusimama kwa wiki tatu kupisha michuano ya CECAFA Challenge Cup iliyofanyika nchini Kenya na mechi za raundi ya pili ya Azam Sports Federation Cup (ASFC).
VPL inaendelea tena leo Ijumaa usiku Desemba 29, 2017 kwa Azam FC kuikaribisha Stand United kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam katika mchezo utakaopigwa kuanzia saa Saa 1:00 usiku.

Kesho Jumamosi Desemba 30, Lipuli na Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa kuanzia saa 8:00 mchana; Mtibwa Sugar na Majimaji ya Songea zikutana katika Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro wakati Ndanda itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Mechi hizo mbili zitachezwa kuanzia saa 10:00 jioni.

Jumapili, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga watakuwa wageni wa Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni huku Njombe Mji FC na Singida United wakitangulia kwa mchezo utakaoanza 8:00 mchana Uwanja wa Saba Saba, Njombe.
VPL itakamilisha mechi za mzunguko wa 12 katika mechi zitakazopigwa mwakani, Januari mosi  ambako Mbeya City wataikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya  na Mwadui wakiikaribisha Ruvu Shooting zote zikianza kutimua vumbi kuanzia saa 10:00 jioni.


Baada ya mechi hizo, Ligi Kuu itasimama tena kupisha mechi za Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar na raundi ya tatu ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani, kabla ya kuingia kwenye mzunguko wa 13 wa ligi kuanzia Januari 13 na 17, 2018.

No comments:

Post a Comment