Friday 1 December 2017

Dk Mwakyembe Kufunga Tamasha la Karatu 2017

Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Olimpiki Tanzania (TOC) imemuomba Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe kuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa tamasha la Michezo na Utamaduni la Karatu 2017.
Tamasha hilo ambalo hushindanisha michezo mbalimbali pamoja na ngoma za utamaduni na kwaya, litafikia kilele Desemba 23 katika viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu.

Mratibu wa tamasha hilo, Meta Petro amesema leo kwa njia ya simu kuwa,
wanatarajia Dk Mwakyembe ndiye atawafungia tamasha lao hilo, ambalo hufanyika kila mwaka.

Tamasha hilo ambalo huandaliwa na Filbert Bayi Foundation (FBF) kwa kushirikiana na TOC, Chama cha Riadha Karatu na kudhaminiwa na Olympic Solidarity,limekuwa chachu ya kuibua vipaji hasa vya riadha.

Petro anasema kuwa mbali na mbio za kilometa 10 na tano kwa wanaume na wanawake, pia kutakuwa na mbio za kilometa 2.5 kwa watoto, mbio za baiskeli za kilometa 60 kwa wanaume na wanawake kilometa 30, soka na mpira wa wavu.


Anasema kuwa mchezo wa soka na wavu fainali zake zitafanyika siku moja kabla ya kilele cha tamasha hilo, Desemba 22 na zawadi zao zitatolewa siku inayofuata, ambapo Dk Mwakyembe ndiye atakayekabidhi zawadi kwa washindi.

No comments:

Post a Comment