Friday 15 December 2017

TFF Yarekebisha Ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara

Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limefanya marekebisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara na sasa itaendelea mwishoni mwa mweiz huu baada ya kusimama ili kupisha michuano ya Chalenji ambayo inafikia kikomo kesho Jumapili nchini Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TFF, mechi za Ligi Kuu raundi ya 12 zitapigwa Desemba 2 na 31 na zingine zitafanyika Januari mosi mwakani.

Vilevile mechi 16 kati ya 152 zilizobaki za Ligi hiyo zitachezwa kuanzia saa 8:00 mchana. Kwa mujibu wa Kanuni ya 14 (45) ya Ligi Kuu, mchezo wowote wa Ligi Kuu unatakiwa kuchezwa kati ya saa 8:00 mchana, na saa 4:00 usiku.

Uamuzi huo umefanywa ili kuongeza mechi ambazo zinataoneshwa moja kwa moja (live) na mdhamini wa matangazo, hatua ambayo itaisaidia Bodi ya Ligi kufuatilia kwa karibu uchezeshaji wa waamuzi na pia kutoa nafasi kwa wadhamini wa Ligi pamoja na wa klabu kuonekana zaidi (mileage).

Hivyo, mechi 102 kati ya 152 zitaoneshwa moja kwa moja ikiwemo zile zinazofanyika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ambazo kwa kawaida zinachezwa kuanzia saa 1:00 usiku.

Mechi za raundi ya 12 ni Desemba 29; Azam vs Stand United (saa 1 usiku), Desemba 30; Lipuli vs Tanzania Prisons (saa 8 mchana), Mtibwa Sugar vs Majimaji (saa 10 jioni), 

Ndanda vs Simba (saa 10 jioni), Desemba 31; Njombe Mji vs Singida United (saa 8 mchana), Mbao vs Yanga (saa 10 jioni), Januari 1; Mbeya City vs Kagera Sugar (saa 10 jioni), na Mwadui vs Ruvu Shooting (saa 10 jioni).

Baada ya raundi ya 12, Ligi Kuu ya Vodacom itapisha mechi za Kombe la Mapinduzi na raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia raundi ya 13 itakayofanyika kati ya Januari 13 na 17, 2018.

Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL), itaingia raundi ya 10 Desemba 30 kwa mechi za Kundi A na C, wakati mechi za Kundi B zitafanyika Desemba 31.

Fainali ya Michuano ya Kombe la Chalenji inafanyika leo nchini Kenya wakati wenyeji Harambee Stars watakapotoana jasho na timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes.

No comments:

Post a Comment