Thursday, 14 December 2017

Wanariadha kibao wajitokeza mbio za Karatu 2017

 
Na Mwandishi Wetu

WANARIADHA na klabu mbalimbali za riadha zimejitokeza kwa wingi kuthibitisha kushiriki tamasha la 16 la Michezo na Utamadani la Karatu litakalofanyika Desemba 23, imeelezwa.

Mratibu wa tamasha hilo linalofanyika kila mwaka mjini humo, Meta Petro alisema leo kwa njia ya simu kuwa, wanariadha binafsi au klabu zimethibitisha kushiriki tamasha hilo, ambalo litamalizikia katika viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu.

Petro alitaja baadhi ya klabu za riadha zilizothibitisha kushiriki kuwa ni pamoja na Magereza Arusha, ambayo itakuwa na wanariadha 20, Jeshi la Kujenga Taifa, Jambo Athletics Club, Ketra zote za Arusha, Lingwa ya Singida na Lyan ya Mbulu.

Mbali na riadha, Petro alizitaja klabu za baiskeli zilizothibitisha kushiriki kuwa ni pamoja na Lake Manyara Cycling Club ya Manyara, Hakika ya Arusha , Klabu ya Baiskeli ya Magugu na Arusha Cycling Club kutoka mkoani humo.

Mbali na riadha na baiskeli, tamasha hilo pia litakuwa na mpira wa wavu pamoja na soka, ambazo fainali zake zitafanyika Desemba 22 ikiwa ni siku moja kabla ya kilele cha tamasha hilo, ambalo litafungwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe.

Petro alisema kuwa pia kutakuwa na burudani za ngoma za utamaduni, kwaya pamoja na maigizo na sarakasi vitakavyofanyika wakati wa ufungaji wa tamasha hilo la kila mwaka.

Wanariadha watachuana katika mbio za kilometa 10 na tano kwa wanaume na wanawake huku watoto wadogo wakichuana katika mbio za kilometa 2.5 wakati mbio za baiskeli zitakuwa za kilometa 60 kwa wanaume wakati wanawake watapiga pedari umbali wa kilometa 30.


Tamasha hilo ambalo huandaliwa na Filbert Bayi Foundation (FBF) kwa kushirikiana na TOC, Chama cha Riadha Karatu na kudhaminiwa na Olympic Solidarity,limekuwa chachu ya kuibua vipaji hasa vya mchezo wa riadha.

No comments:

Post a Comment