Friday 1 December 2017

Bondia Anthony Joshua ataka umaarufu wa Federer

LONDON, England
NYOTA wa ndondi za uzito wa juu wa Uingereza, Anthony Joshua anataka kujijengea umaarufu katika ndondi za kulipwa kama ule wa Roger Federer katika mchezo wa tenisi.

Joshua hadi sasa ameshinda mapambano 20-0, yote yakiwa kwa KO na kumpatia umaarufu mkubwa katika mchezo huo.

Bondia huyo tayari ameweka rekodi ya kuingiza watazamaji wengi katika moja ya mapambano yake, likiwa limeingiza watazamaji 90,000 Aprili mwaka huu alipomsimamisha Wladimir Klitschko kwenye Uwanja wa Wembley hapa.

Baadae pambano lake jingine lililofanyika mwezi uliopita, liliingiza watazamaji 78,000, ambalo lenyewe alishinda kwa TKO dhidi ya bondia Carlos Takam lililofanyika kwenye Uwanja wa Manispaa wa Cardiff, Wales.

Kuna wataalamu wengi wanaamini kuwa bingwa huyo wa dunia wa WBA, IBF na IBO atakuwa mwiba mkali katika ngumi.

Federer, bingwa mara 19 wa mataji makubwa, anachukuliwa kwa kiasi kikubwa kuwa ni mcheza tenisi mkubwa zaidi katika kipindi chote na Joshua ana nia hiyo ya kujiweka katika nafasi hiyo.

"Sasa naelewa, natakiwa kucheza ndondi ikiwa nataka kujijengea jina, “alisema bondia huyo Muingereza mwenye umri wa miaka 28.

"Bado sijatekeleza jukumu langu. Lakini angalia bondia kama Muhammad Ali, ambaye amekuwa alama ya mchezo wa ndondi….”

"Ikiwa unataka kuwa watu kama hawa, unatakiwa kujibidiisha katika njia sahihi.

"Nataka kuwa kama akina [Cristiano] Ronaldos, [Lionel] Messis, Federers anayeshindana na [Rafael] Nadal, [Andy] Murray. Hilo nataka kulipeleka katika ngumu.”

No comments:

Post a Comment