Monday 25 December 2017

Serikari yawakoromea Maofisa Michezo, Utamaduni

Na Mwandishi Wetu, Karatu


SERIKALI imesema kuwa maofisa michezo na wale wa utamaduni hawafanyi kazi zao vizuri na ndio maana kumeshindwa kuvumbuliwa vipaji vipya na kusababisha wachezaji wale wale kushiriki katika mashindano mara kwa mara.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifunga tamasha la 16 la Michezo na Utamaduni la Karatu kwenye viwanja vya Mazingira Bora hapa.

Shonza alisema kuwa maofisa michezo na utamaduni wengi wao wamekuwa wakipokea mishahara bure, kwani wameshindwa kufanya kazi zao za kusaidia kuibua vipaji kama wanavyofanya wenzao wa Karatu kupitia tamasha hilo.

Alisema maofisa hao wanatakiwa kwenda chini hatua ya vijiji ili kuibua vipaji na kuviendeleza tofauti na wengi wao, ambao wanapokea mishahara bure bila ya kufanya kazi yoyote.

Aliongeza kusema kuwa ndio maana vijana wengi wamekuwa wakijihusisha na shughuli zisizofaha kama uvutaji wa bangi, matumizi ya dawa za kulevya na wizi kutokana na kutoshirikishwa katika michezo, hivyo aliwataka maofisa hao kufanya kazi zao vizuri.

Pia aliwataka viongozi wa wilaya ya Karatu kuhakikisha wilayani kwao kuna kiwanja kikubwa cha michezo ili kuwawezesha vijana kutumia kiwanja hicho kuendeleza vipaji vyao.

Alisema ni aibu kubwa kuona wilaya ya Karatu pamoja na vipaji vya michezo vilivypo hakuna uwanja wa maana wa michezo, hivyo aliwataka kukijenga au kuwapokonya wale waliovamia maeneo ya wazi.


No comments:

Post a Comment