Saturday 30 December 2017

Simba Yarejea Kileleni Ligi Kuu Tanzania Bara

Na Mwandishi Wetu
SIMBA leo imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuifunga Ndanda FC mabao 2-0  katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Alikuwa ni mshambuliaji John Bocco aliyepeleka kilio kwa Ndanda FC iliyokuwa inacheza mbele ya mashabiki wake baada ya kufunga mabao yote mawili katika kipindi cha pili baada ya dakika 45 kumalizika kwa suluhu.

Bao la kwanza alilifungwa dakika ya 52 kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona iliyopigwa na Shiza Kichuya na bao la pili alilifunga katika dakika ya 56 akitumia makosa ya mabeki wa Ndanda na kipa wao, Jeremiah Kisubi kuzembea kuokoa mpira mrefu ulioingizwa kwenye eneo la hatari.


Ndanda walijitahidi kupeleka mashambulizi kwenye eneo la Simba, wakiongozwa na mkongwe Mrisho Ngassa, lakini umaliziaji mbovu ukawakosesha kupata bao la kufuta machozi.

Kwa ushindi huo, Simba inafikisha pointi 26 baada ya kucheza mechi 12, sawa na Azam FC walio nafasi ya pili kwa kuzidiwa wastani wa mabao.

Azam FC juzi waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wao wa Chamazi Mbagala jijini Dar es Salaam.

Yanga  wenye pointi 21 ambao leo wanashuka dimbani wataendelea kushika nafasi ya tatu endapo watashinda dhidi ya Mbao FC kama watatoa sare au kupoteza na Singida United wakishinda dhidi ya Njombe Mji FC, basi watashuka hadi nafasi ya nne.

Katika Uwanja wa Samora Iringa jana, Tanzania Prisons waliifunga Lipuli FC bao 1-0 lililofungwa na Salum Kimenya na Mtibwa Sugar iliifunga Majimaji mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Manundu Turiani, Morogoro.

Kikosi cha Ndanda FC kilikuwa, Jeremiah Kisubi, William Lucian, Abdallah Suleiman/Ayoub Masoud dakika 51, Ibrahim Job, Hamad Waziri, Hemed Khoja/Omar Mponda dakika 61, Jacob Massawe, Majid Khamis, John Tibar/Alex Sethi dakika 72, Jabir Aziz na Mrisho Ngassa.


Kikosi cha Simba ni Aishi Manula, Paul Bukaba, Shiza Kichuya, Juuko Murshid, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, John Bocco, James Kotei/Yussuf Mlipili dakika 72, Juma Luizio/Moses Kitandu dakika 54, Muzamil Yassin na Mohamed Ibrahim ‘Mo’/Said Ndemla dakika 38.

No comments:

Post a Comment