Tuesday 19 December 2017

Zawadi Zaongezwa Tamasha la Karatu 2017

Na Mwandishi Wetu
WAANDAAJI wa tamasha la kila mwaka la michezo na Utamaduni la Karatu wameongeza zawadi kwa washindi watatu wa kwanza wa michezo yote itakayoshindaniwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo Meta Petro, bingwa wa mwaka huu wa mbio za kilometa 10 kwa wanaume ataondoka na kitita cha sh 500,000 huku mshindi wa pili akipata sh 300,000 wakati watatu ataondoka na sh 250,000.

Zawadi kama hizo pia zitatolewa kwa washindi wa kwanza hadi watatu wa mbio za wanawake za kilometa tano, huku watoto wadogo, ambao watashiriki mbio za kilometa 2.5, wenyewe mwaka huu mshindi wa kwanza, ataondoka na sh 100,000 badala ya 50,000.

Mbali na riadha, pia zawadi kwa washindi wa mbio za baiskeli ambazo zitawashindanisha wanaume katika umbali wa kilometa 60 na wanawake 30, nao mwaka huu wameongezewa zawadi.

Mbali na mbio na baiskeli, pia tamasha hilo linashirikisha mchezo wa soka, mpira wa wavu, kwaya pamoja na ngoma za utamaduni na sarakasi.

Alisema kuwa tamasha la mwaka huu linatarajia kuvuta washiriki wengi baada ya klabu kibao na wanariadha binafsi na wapanda baiskeli kujisajili kwa wingi kwa ajili ya kushiriki michezo hiyo.

Baadhi ya klabu za riadha ambazo zimethibitisha kushiriki tamasha hilo ni pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),ambayo itakuwa na zaidi ya wanariadha 25, Magereza Arusha yenye anariadha 20, Jambo Athletics Club, Ketra zote za Arusha, Lingwa ya Singida na Lyan ya Mbulu.

Mbali na riadha, Petro alizitaja klabu za baiskeli zilizothibitisha kushiriki kuwa ni pamoja na Lake Manyara Cycling Club ya Manyara, Hakika ya Arusha , Klabu ya Baiskeli ya Magugu na Arusha Cycling Club kutoka mkoani humo.

Mbali na riadha na baiskeli, tamasha hilo pia litakuwa na mpira wa wavu pamoja na soka, ambazo fainali zake zitafanyika Desemba 22 ikiwa ni siku moja kabla ya kilele cha tamasha hilo, ambalo linatarajia kufungwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe.


Tamasha hilo ambalo huandaliwa na Filbert Bayi Foundation (FBF) kwa kushirikiana na TOC, Chama cha Riadha Karatu na kudhaminiwa na Olympic Solidarity,limekuwa chachu ya kuibua vipaji hasa katika mchezo wa riadha.

No comments:

Post a Comment