Friday 15 December 2017

Zanzibar Heroes Yaivua Ubingwa Uganda Cranes


Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, imeivua ubingwa wa Kombe la Chalenji Uganda Cranes baada ya kuifunga mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Moi mjini Kisumu leo.

Zanzibar ambayo awali ilikuwa haipewi nafasi ya kufanya vizuri, iliwavua ubingwa Uganda katika mchezo huo wa nusu fainali ya pili na sasa itakutana na wenyeji Kenya katika mchezo huo wa fainali.

Hii ni mara ya pili kwa Zanzibar kucheza nusu fainali baada ya mara ya kwanza kufikia hatua hiyo mwaka 1995, ambapo ilitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza.

Mchezaji wa Zanzibar, Abdul-Azziz Makame ndiye aliyeifungia timu hiyo bao la kwanza katika dakika ya 22 kabla mfungaji anayeogoza kwa kupachika mabao katika mashindano hayo, Derrick Nsibambi kuisawazishia Uganda na kufikisha mabao manne dakika saba kabla ya mapumziko.

Mohammed Issa Juma ndiye aliyeihakikishia Zanzibar Heroes kucheza fainali na kunusa ubingwa baada ya kufunga bao la ushindi  kwa penalty baada ya dakika 57 na kuiwezesha timu hiyo ya kisiwani kuweka historia ya ushindi mjini Kisumu.

Sasa sasa watacheza na wenyeji Harambee Stars – ambao waliifunga Burundi kwa bao baada ya muda wa nyongeza katika nusu fainali ya kwanza baada ya timu hiyo kutoka suluhu katika dakika 90 za kawaida na kuongezewa dakika zingine 30 kwenye Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos.
Fainali hiyo itapigwa Jumapili, ambapo mshindi atapatikana.

The Cranes walimaliza wakiwa 10 uwanjani baada ya mchezaji aliyeingia akitokea benchi, Joseph Nsubuga alipotolewa nje baada ya kuonyeshwa kadi yekundu ya moja kwa moja katika dakika ya 55 baada ya kumchezea vibaya Ahmada Ibrahim katika eneo la hatari.

“Huu ulikuwa mchezo mgumu dhidi ya mabingwa watetezi, Namshukuru Mungu na wachezaji wangu kwa ushindi huu uliotupeleka katika fainali ya Cecafa Challenge Cup. Tulistahili kushinda leo kutokana na jinsi tulivyocheza.”


“Tunaiheshimu Kenya ambao ni wapinzani wetu wajao katika fainali. Na hiyo haina maana kuwa tunawaogopa bkwa sababu tumekuja hapa kushinda kikombe.” Alisema kocha wa Zanzibar Hemed Morocco.

No comments:

Post a Comment