Friday 15 December 2017

Mabondia Timu ya Taifa Walilia Kambi, Vifaa

Na Mwandishi Wetu
MABONDIA wa timu ya taifa ya Tanzania wamesema kuwa wanataka kupatiwa kambi ya kudumu pamoja na vifaa ili waweze kujiandaa vizuri kwa ajili ya Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Aprili mwakani Gold Coast, Australia.

Kocha Mkuu wa timu hiyo inayoendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, Said Omary au maarufu kama Gogopoa alisema juzi kuwa timu inaendelea na mazoezi lakini ina changamoto kibao.

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na mabondia kukosa vifaa vya mazoezi zikiwemo padi, glovu na vifaa vingine pamoja na kutokuwa katika kambi ya kudumu na hivyo kushindwa kufuatilia mazoezi vizuri.

Amesema anaiomba Serikali kuingia kati suala hilo ili timu hiyo ipate mahitaji yake na iweze kujiandaa vizuri kwa ajili ya michezo hiyo ya mwakani.

Naye nahodha wa timu hiyo, Seleman Kidunda alisema kuwa mabondia wanahitaji kambi ya kudumu ili kuwapunguzia gharama za kwenda na kurudi kutoka mazoezini.

Alisema mbali na nauli, mabondia hawana fedha za kupata mlo baada ya mazoezi na timu hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya mazoezi,

Pia Kidunda amesema kuwa pia mabondia wanahitaji mechi za majaribio ili kuwaweka fiti na kuwapatia uzoefu kwa ajili ya mashindano ya kimataifa.


Juhudi za kuwapata viongozi wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT) zinaendelea baada ya simu ya katibu mkuu wake, Makore Mashaga kuitwa bila kupokelewa leo.

No comments:

Post a Comment