Thursday 12 January 2017

DStv KUONESHA FAINALI ZA AFCON GABON 2017 KWA BEI MCHEKEA!



Multchoice-Tanzania Wahakikisha shoo ya Diamond inafunika
 
Jumatano January 11, 2017

ILI kuwapa watanzania wengi uhakika wa kushuhudia michuano ya kombe Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017, 

Kampuni ya Multichoice Tanzania kupitia king’amuzi chake maarufu cha DStv, itaonyesha michuano hiyo katika kifurushi chake cha bei ya chini kabisa maarufu kama DStv Bomba. Kifurushi hicho kinachopatikana kwa bei ya sh 19,975 tu, ni miongoni mwa vifurushi vya bei nafuu katika huduma ya ving’amuzi hapa nchini.

Akizungumza katika mkutano na waandisha wa habari leo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa  Multichoice Tanzania Salum Salum, ametanabahisha kuwa kwakuwa DStv ndicho king’amuzi pekee kitakachoonyesha michuno hiyo mubashara kupitia chaneli yake ya michezo ya SuperSport4 (DStv 204), wameamua kuiweka michuano hiyo kwenye kifurushi cha bei nafuu kabisa cha Bomba, ili kuwawezesha watanzania wengi zaidi kuiona michuano hiyo moja kwa moja.

“Tunajivuna kuwa na sisi Tanzania tumepiga hatua kubwa sana na sasa hatuna sababu yoyote ya kuona michezo iliyerekodiwa, bali na sisi tunaitazama mubashara kupitia king’amuzi chetu bora cha DStv, tena kwenye kifurushi nafuu cha Bomba” alisema Salum na kuongeza kuwa kwa kuwa hii itawapa nafasi watanzania wengi kufurahia michuano hiyo kila mahali ikiwemo kwenye kumbi za burudani na hata majumbani.

Wakati huohuo, DStv na Wizara ya Habari Utamaduni Michezo na Sanaa, imefanikisha safari ya Mwanamuziki wa kizazi kipya hapa nchini Nasibu Abdul (Diamond) katika kufanikisha onyesho lake katika ufunguzi wa mashindano ya AFCON nchini Gabon.

Diamond ni miongoni mwa wasanii teule watakaotumbuiza katika hafla hiyo kitendo ambacho kimechukuliwa na watanzania wengi kuwa ni fursa ya Tanzania kusikika katika mashindano hayo japokuwa timu yetu haikuweza kufuzu kushiriki.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, utamaduni, michezo na sanaa Nape Nnauye alisema kuwa kuwepo kwa Diamond kwenye uzinduzi wa michuano hiyo ni kitendo cha kujivunia na kwamba serikali ikishirikiana na DStv imefanya jitihada kubwa kufanikisha safari ya WCB kuelekea Gabon.  

Kwa upande wake Diamond aliishukuru Serikali na DStv kwa ushirikiano wao hususan kufanikisha safari yao ya kuelekea Gabon. Aliongeza kuwa jitihada binafsi za Waziri wa Habari ziliwezesha zoezi hilo kufanikiwa na kwamba wanaahidi kuwa hawaendi kama WCB, bali kama watanzania na watahakikisha kuwa wanaipeperusha vema bendera ya Tanzania katika onyesho hilo.

Michuano ya AFCON ya mwaka huu inanogeshwa zaidi na uwepo wa wachezaji nguli ulimwenguni hususan wale wanaochezea vilabu vikubwa kama Manchester United, Arsenal, Chelsea, Real Madrid na vilabu vingine vikubwa duniani. Wababe wa kabumbu kama Mohamed Elneny, Eric Bailly, John Obi Mikel, Pierre Aubemayang, Riyad Mahrez, Sadio Mane na Victor Moses ni miongoni mwa vigogo watakaoonyesha umahiri wao katika michuano hiyo.

Mtifuano huo wa AFCON mwaka huu unafanyika katika nchi ndogo ya Gabon, huku jumla ya timu 16 zikishiriki ikiwemo Uganda ambayo ndiyo timu pekee iliyofuzu kutoka Afrika Mashariki.

Tayari vuguvugu la michuani hiyo limeshaanza kushika kasi mitaani ambambo mashabiki wa timu mbalimbali wamekuwa wakitambiana kila mmoja akidai timu yake itanyakua ubingwa mwaka huu. 

Michuona ya AFCON 2017 inadhaminiwa na kampuni ya Total, na itaanza tarehe 14 January na fainali itakuwa tarehe 05 Februari. Tayari ratiba kamili ya michuano hiyo imeshatolewa na inapatikana katika tovuti ya www.dstv.com.

No comments:

Post a Comment