Sunday, 1 January 2017

WATU 39 WAUAWA KATIKA SHAMBULIZI LA KIGAIDI KATIKA KLABU YA USIKU JIJINI ISTAMBULI MKESHA WA MWAKA MPYA 2017

ISTAMBULI, Uturuki
KWA uchache watu 39, wakiwemo wageni 16, wamekufa katika shambulizi lililofanyika katika klabu ya usiku jijini hapa. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki amesema.

Suleyman Soylu pia alibainisha kuwa,  Polisi bado wanawasaka “magaidi” hao waliofanya shambulizi hilo katika klabu hiyo ya usiku ya Reina kwa saa 7:30 usiku kwa saa za hapa.

Hatahivyo, kwa saa kadhaa baada ya shambulio hilo, mamlaka za taifa zilikuwa kimya kuhusu suala hilo.

Watu wengine 69 walipatiwa matibabu hospitalini, alisema waziri huyo.

"Usakaji wa magaidi hao bado unaendelea…Natarajia (washambuliaji) watakamatwa haraka kwa mapenzi ya Mungu, “ alisema Soylu.

Mamlaka ya Uturuki imevizuia vyombo vya habari kuripoti shambulio hilo, lakini alizuii taarifa za viongozi.

Gavana wa Jiji la Istanbul, Vasip Sahin awali alibainisha kuwa ofisa wa polisi alikufa katika shambulio hilo.
Pia mshambuliaji mmoja alihusi, alisema gavana huyo, wakati Kituo cha Televisheni cha CNN cha Uturuki kiliripoti kuwa, mshambuliaji huyo alivalia vazi la Father Krismas .

"Magaigi wakiwa na silaha…walifanya vitendo vya kikatili ikiwemo kuwafyatulia risasi raia wema na watu wengine waliokuwa wakisheherekea  Mwaka Mpya na kucheza, “alisema Sahin alipozungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio katika eneo la Ortakoy.

Klabu hiyo sio maarufu tu kwa Waturuki, bali pia hata kwa wageni kutoka nje ya nchi, ambao walipenda kwenda kula bata, kwa mujibu wa Mtangazaji wa Shirika la Utangazji la Uingereza la BBC, Selin Girit jijini Istanbul.

Aliongeza kuwa watu walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa washambuliaji walikuwa wawili.
Iliripotiwa kuwa ndani ya klabu hiyo ya usiku kulikuwa na watu zaidi ya 700 wakati shambulio hilo likitokea, ambapo baadhi yao walirukia katika maji ili kujiokoa.

Shirika la Habari la Dogan liliriopit kuwa baadhi ya mashuhuda walidai kuwa baadhi ya washambuliaji hao walikuwa “wakizungumza Kiarabu” wakati channeli ya Televisheni ya Uturuki ya NTV ilisema polisi maalum walikuwa wakipekuwa klabu hiyo ya usiku.

Rais wa Marekani Barack Obama, ambaye yuko katika mapumziko huko Hawaii, ni miongoni mwa viongozi wa kwanza wa kimataifa kutoa taarifa baada ya kutaarifiwa na timu yake.

"Rais ametuma salamu za rambirambi kwa kupotea kwa maisha ya watu wasio na hatia…”ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Obama iliyotolewa na msemaji wa Ikulu ya Marekani Eric Schultz.

Serikali ya Uturiki imetoa amri ya kuzuia kwa muda vyombo vya habari vya hapa kuripoti taarifa hizo, kutokana na suala la kiusalama.

Hii sio mara ya kwanza kwa amri kama hiyo kutolewa.

Istanbul ilikuwa katika hali ya taadhari huku kukiwa na askari polisi zaidi ya 17,000 wakiwa kazini jijini hapa, kufuatia kuwepo na matukio kadhaa ya kivamizi katika miezi ya hivi karibuni.

Vitendo vingi vya kigaidi vimekuwa vikifanywa na Dola ya Kiislamu (IS) na wale wanaofahamika kama askari wa Kikurdi.

Chini ya wiki mbili, Balozi wa Urusi nchini hapa,  Andrei Karlov, aliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Uturuki ambaye hakuwa kazini Mevlut Mert Altintas wakati akihutubia katika jiji la Ankara mwezi uliopita.

Baada ya mauaji hayo muuaji alikuwa akipiga kelele kuwa kitendo hicho ni kulipa kisasi kwa Urusi kujiingiza katika mgogoro katika jiji la Syria la Aleppo.

Mashambulizi makubwa Uturuki kwa mwaka 2016

Desemba 10: Mashambulizi mawili ya mabomu yalifanyika nje ya uwanja wa soka jijini Istanbul na kuua watu 44, kundi la askari wa Kikurdi walidai kuhusika ba tukio hilo.

Agosti 20: Shambulizi la bomu katika sherehe ya harusi huko Gaziantep liliua watu 30, huku kundi la IS likihisiwa kuhusika.

Julai 30: Wapiganaji 35 wa Kikurdi walijaribu kuvamia ngome ya kijeshi na kujikuta wakiuawa na Jeshi la Uturuki.

Juni 28: Shambulio la risasi na bomu katika uwanja wa ndege wa Ataturk jijini Istanbul viliua watu 41, katika shambulio lililodaiwa kufanywa na askari wa IS.

Machi 13: Watu 37 waliuawa na askari wa Kikurdi katika bomu kurushwa katika gari jijini Ankara.
Februari 17: Watu 28 walikufan katika shambulio jijini Ankara.

No comments:

Post a Comment