Sunday, 22 January 2017

Ghana yasonga mbele wakati Uganda ikiaga mashindano Gabon 2017


WAKATI Ghana ikitinga robo fainali ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika yanayoendelea Gabon, wawakilishi wa Afrika Mashariki Uganda wametolewa.

Asamoah Gyan aliiongoza Ghana katika hatua inayofuata ya mtoano baada ya kuifungia bao lililoiwezesha timu hiyo kuibuka na ushindi dhidi ya Mali kwa bao 1-0 katika mchezo uliopigwa mapema juzi.

Gyan alifunga bao hilo pekee katika mchezo huo wa Kundi D kwa kichwa katika mchezo uliofanyika hapa.

Katika mchezo mwingine, mabingwa wa kihistoria wa kombe hilo, Misri wenyewe walimtumia mchezaji aliyetokea benchi Abdallah El Said na kufunga katika dakika ya 89 na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Uganda.
Kwa kipigo hicho, Uganda ndio imekuwa timu ya kwanza kabisa kukata tiketi ya kurudi nyumbani.

Ghana ambao ni mabingwa mara nne, ambao walimaliza katika nafasi ya pili mwaka 2015, ni timu pekee ya pili ya kufuzu kwa robo fainali, wakati nyingine ni Senegal.

"Katika mashindano unahitajika kushinda mechi na hilo ndilo tulilofanya leo, alisema Gyan, ambaye sasa amefunga katika fainali sita za Mataifa ya Afrika.
"Tumeridhishwa na kiwango chetu. Ama tumecheza mchezo mzuri au la, muhimu ni kushinda na kusonga mbele."

Baada ya ushindi mfululizo wa baoa 1-0, kikosi cha kocha Avram Grant kitamaliza cha kwanza endapo kitakwepa kufungwa wakati watakapocheza na Misri katika mchezo wa mwisho wa kundi lao utakaofanyika keshikutwa Jumatano.

Timu zilizuiwa kufanya mazoezi kabla ya kuanza kwa mechi ili kuepuka kuharibuka zaidi eneo la kuchezea, ambapo mchezo ulipoanza Ghana ndio walizoea haraka hali ya mchezo.
Andre Ayew nusura afunge bao baada ya kupata pasi safi kutoka kwa Christian Atsu lakini alipiga juu, kabla bao pekee halijafungwa katika dakika ya 21.

Gyan alifunga kwa akichwa akiunganisha krosi ya Jordan Ayew likiwa ni bao lake la nane katika mashindano ya Mataifa ya Afrika, ambapo bao lake la kwanza alilifunga mwaka 2008 wakati fainali hizo zilipofanyikia Ghana.

Mali, ambao walitolewa katika hatua ya makundi baada ya kutoka sare nyingi mwaka 2015, sasa wanatakiwa kuifunga Uganda katika mchezo wa mwisho na huku wakiombea kufungwa kwa Misri kama wanataka kuendelea kuwepo katika mashindano.
Misri wenyewe wanahitaji pointi moja tu ili kujihakikishia nafasi ya kucheza hatua inayofuata baada ya ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya Uganda Jumamosi usiku.

Kikosi cha kocha Hector Cuper kilitoka suluhu na Mali katika mchezo wao wa kwanza na baadae kuonekana kama ingetoka tena sare ya bila kufungana hadi pale Mohamed Salah alipomtengenezea mchezaji aliiyetokea benchi El Said aliyefunga bao hilo.

Ni pigo kwa Uganda ambao walifungwa kwa penalty katika mchezo wa kwanza dhidi ya Ghana na kujikuta wakimaliza mchezo wakiwa nyuma kwa bao 1-0 baada ya juzi kushindwa kuondoka na pointi hata moja.


Wakiwa mkiani bila ya pointi hata moja, katika fainali zake za kwanza za Afcon tangu iliposhiriki kwa mara ya mwisho mwaka 1978 wataishia katika hatua ya makundi, bila kujali watapata matokeo gani dhidi ya Mali katika mchezo utakaofanyika Oyem kesho.

No comments:

Post a Comment