Friday, 13 January 2017

Taifa Stars yapangwa kundi jepesi kinyang'anyiro cha kufuzu Mataifa ya Afrika Cameroon 2017


Na Mwandishi Wetu
 ALIYEKUWA Kocha wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ Charles Mkwasa amesema kilio chake kimesikika na hatimaye Tanzania imepangwa kwenye kundi rahisi kuwania kufuzu Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2019.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkwasa ambaye ameifundisha Taifa Stars akirithi mikoba ya kocha Mdenmark Mart Nooij amesema timu ambazo zipo kundi moja na Tanzania ni rahisi ukilinganisha na kundi la msimu uliopita ambapo ilipanga na Nigeria na Misri.

“Timu zilizopangwa kundi moja na Tanzania ni timu za kawaida ukilinganisha na Misri au Nigeria lakini maandalizi ya mapema ni muhimu ili kufanya vizuri,” alisema Mkwasa.

Pia Mkwasa alisema pamoja na kuonekana kuwa rahisi lakini kitendo cha nchi hizi kuwa na viwango vinavyokaribiana kinaweza kufanya iwe ngumu zaidi kwa maana ya kukamiana.

“jukumu linabaki kwa shirikisho la Soka (TFF), wachezaji pamoja na benchi la kiufundi kujiandaa kwani nilisema hadharani tumekuwa tukipangwa kwenye kundi la kifo ila droo ya sasa CAF walisikia kilio changu na inawezekana iwapo tutaamua,” alisema Mkwasa.

Tanzania imepangwa Kundi L pamoja na vinara wa soka ukanda wa Afrika Mashariki Uganda, Lesotho na Cape Verde, ambapo wengi wanasema ni jepesi ukilinganisha na huko nyuma ilibyokuwa ikipangwa Stars.

Kwa upande wa timu ya Taifa ya Kenya 'Harambee Stars' ambayo ipo ukanda huu wa Afrika Mashariki imepangwa kundi F sambamba na Ghana, Ethiopia na Sierra Leone.

Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema ratiba hiyo ni faraja kubwa kwa Tanzani kwani wadau wa soka wakiungana na TFF, “hakuna shaka tunaweza kufuzu kwa fainali hizo za 2019.”

Hatahivyo,Lucas alisema pamoja na kuwepo katika kundi linaloonekana jepesi, lakini bado maandalizi ya Stars yanatakiwa kuwa makubwa kwani Uganda na Cape Verd bado ni timu nzuri.

Alisema kuwa Uganda Cranes ni timu nzuri na itakuwa na hamu kubwa ya kucheza tena fainali hizo za mwaka 2019 baada ya kushiriki zile za mwaka huu nchini Gabon, ambazo zinaanza leo.

Wenyeji wa michuano hiyo Cameroon ambayo imefuzu moja kwa moja imepangwa kundi B pamoja na Morocco, Malawi na mshindi kati ya Comoro na Mauritius.

Wakati huo huo;  timu za Sao Tomé, Madagascar, Comoro, Mauritius, Djibouti na Sudan Kusini wataanzia kwenye mechi za mtoano Machi na mataifa matatu yataingia kwenye hatua za makundi.

Jinsi makundi yalivyopangwa:

Kundi A: Senegal, Equatorial Guinea, Sudan, Sao Tome/Madagascar

Kundi B:  Cameroon, Morocco, Malawi, Comoro/Mauritius

Kundi C: Mali, Gabon, Burundi, Djibouti/Sudan Kusini.

Kundi D: Algeria, Togo, Benin Gambia.

Kundi E: Nigeria, Afrika Kusini, Libya, Shelisheli.

Kundi F: Ghana, Ethiopia, Sierra Leone, Kenya.

Kundi G: DR Congo, Congo Brazzaville, Zimbabwe, Liberia.

Kundi H: Ivory Coast, Guinea, Jamhuri ya Afrika ya kati, Rwanda

Kundi L: Burkina Faso, Angola, Botswana, Mauritania.

No comments:

Post a Comment