Wednesday 11 January 2017

Waziri Nape ampongeza Diamond Platnumz kupata nafasi ya kutumbuiza ufunguzi wa Afcon Gabon na ameishukuru Multchoice kutoa tiketi




Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye (kushoto) akimkabidhi bendera ya taifa Diamond Platnumz wakati wa hafla ya kuaga iliyofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Multchoice- Tanzania, Salum Salum (kulia) na Msanii Joti.

 Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amempongeza mwanamuziki wa Tanzania Nassib Abdul au Diamond Platnumz kwa kupata nafasi ya kutumbuiza katika ufunguzi wa fainali za Mataifa ya Afrika, Afcon.
Nape pia ameipongeza Multchoice-Tanzania kwa kutoa tiketi sita kumuwezesha Diamond na wasanii wake kwenda Gabon kutumbuiza katika ufunguzi wa fainali hizo za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika nchi humu kuanzia Jumamosi Januari 14 hadi Februari 15, ambapo timu kutoka Mataifa 16 zitatifuana katika patashika hiyo.
 
Nape akizungumza katika hafla ya kumkabidhi bendera ya taifa Diamond jijini Dar es Salaam jana katika hoteli ya Serena alisema kuwa, kitendo cha msanii huyo kwenda kutumbuiza katika ufunguzi huo ni heshima kubwa kwa Tanzania.

Alimtaka Diamond kuliwakilisha vizuri  taifa licha ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kutopata nafasi ya kushiriki fainali hizo.
 
Nape pia aliishukuru Multchoice-Tanzania kwa kukubali kuwapatia tiketi sita wasanii wa Diamond ili kwenda kunogesha shoo hiyo ya mwanamuziki huyo mwenye mafanikio makubwa nchini.

Alisema nafasi ya Diamond angeweza kupewa msanii mwingine yoyote nyota kutoka katika nchi zinazojiita mahiri katika tasnia hiyo, na badala yake alipewa Mtanzania huyo.

Alisema hiyo ni fursa kubwa kwa Diamond kuitangaza Tanzania kimataifa katika muziki.

Naye Diamond alimshukuru Nape kwa kupiga hodi Multchoice na kuwaombea tiketi wasanii wake.

Kaimu Mkurugenmzi Mtendaji wa Multchoice- Tanzania, Salum Salum alisema Afcon ni uhondo mwingine kwa Watanzania kwani DStv ndio chaneli pekee itakayoonesha fainali hizo.

Alisema Diamond ataendelea kupata nafasi za kutumbuiza katika hafla mbalimbali za michezo na alimtakia heri ili siku moja aje kutumbuiza katika fainali za Kombe la Dunia.
Kaimu Mkurugenzi wa Multchoice-Tanzania, Salum Salum.
 “DStv ndio itakuwa chaneli pekee yenye ruksa ya kuonesha fainali hizo za Afco Tanzania na TV nyingine yeyote ikionesha hapa nchini itakuwa inaiba matangazo, “alisema Salum.
Wiki iliyopita Diamond alipata fursa ya kutumbuiza wakati wa utoaji wa tuzo za wachezaji bora wa mwaka wa Afrika zilizoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) zilizofanyika Abuja, Nigeria.

Katika uzinduzi huo, Diamond ataimba kibao maalum pamoja na wasanii Mohombi na Franco, kiba ambacho pia kitakuwa wimbi wa mashindano hayo.

 

 

 

No comments:

Post a Comment