Friday 6 January 2017

Mahrez wa Leicester City ndiye mchezaji bora wa Afrika wa mwaka wa Caf


Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Algeria na Leicester Riyad Mahrez akipozi kwa picha baada ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika katika hafla iliyofanyika jana usiku jijini Abuja, Nigeria.

ABUJA, Nigeria
MSHAMBULIAJI wa Leicester Riyad Mahrez ndiye mchezaji bora wa Afrika kwa mwaka 2016, Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) limetangaza.

Mchezaji huyo wa Algeria mwenye umri wa miaka,25, aliyeisaidia Leicester kutwaa taji la Ligi Kuu ya England, tayari ndiye mchezaji bora wa PFA wa mwaka na yule wa BBC.

Mshambuliaji wa Gabon anayeichezea klabu ya Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang alikuwa wa pili na Msenegal wa Liverpool Sadio Mane alimaliza watatu katika mbio hizo za kuwania uchezaji bora.

Mshambuliaji wa Arsenal na Nigeria Alex Iwobi alishinda tuzo ya mchezaji chipukizi wa mwaka.

Mchezaji mwingine wa Nigeria anayekipiga katika klabu ya Manchester City, Kelechi Iheanacho alikuwemo katika orodha ya wachezaji waliokuwa wakiwania heshima hiyo.

Mahrez, 25, alimshinda nahodha wa Gabon Pierre-Emerick Aubameyang, ambaye alipata heshima hizo mwaka jana, lakini juzi aliishia katika nafasi ya pili.

Mshambuliaji huyo mzaliwa wa Ufaransa alisema kuwa ni heshima kubwa sana kwake kuwa mchezaji bora wa Afrika kwa mwaka uliomalizika.

"Ni heshima kuubwa, nina furaha na ninashukuru. Nawashukuru wachezaji wenzangu wote Leicester na Algeria," alisema Mahrez wakati akipokea tuzo hiyo.

"Natoa tuzo hii kwa familia yangu na wote wanaoniunga mkono kila siku.”

Leicester ilishangaza pale ilipotwaa ubingwa wa England wakati ilikuwa haipewi nafasi yoyote hata ya kubaki katika ligi hiyo msimu uliopita.

Mahrez alifanya kazi kubwa katika klabu yake baada ya kufunga mabao 17 na ksaidia kupatikana kwa 10 katika mechi 37 alizoichezea timu hiyo.

Alikuwa mchezaji wa kwanza wa Algeria kushinda taji la Ligi Kuu na kupata mapokezi makubwa aliporejea nyumbani Algeria, ambako kwa mara ya kwanza alifikiriwa kuwa ni mchezaji wa rugby alipotakiwa kujiungta na timu hiyo miaka minne iliyopita.

Wachezaji wote watatu waliokuwa wakiwania tuzo hiyo ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika pia walichaguliwa katika kikosdi cha CAF cha wachezaji 11, ambacho pia kinaundwa na beki wa Ivory Coast Eric Bailly wa Manchester United.

Kipa Denis Onyango alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani baada ya kumshinda mchezaji mwenzake wa Mamelodi Sundowns Khama Billiat na Mzambia Rainford Kalaba.

Onyango alifanya vizuri wakati klabu yake ya Mamelodi Sundowns ilipotwaa taji la Ligi ya Mabingwa wa Afrika, na kuisaidia timu ya taifa ya Uganda `The Cranes’ kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), baada ya kutokuwepo kwa muda mrefu.

Mnigeria Asisat Oshoala alitwaa tuzo yake ya pili ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika kwa wanawake baada ya kuisaidia Nigeria kutetea taji la Afrika nchini Cameroon.

Nyota huyo wa timu ya wanawake ya Arsenal alishinda kwa mara ya kwanza tuzo hiyo wakati pia alipoweza kuisaidia Super Falcons kutwaa taji la Afrika mwaka 2014.

Wachezaji chipukizi wa Nigeria Kelechi Iheanacho na Alex Iwobi walitwaa tuzo ya wachezaji wanaochipukia vizuri na ile ya wachezaji chipukizi wa mwaka.

Mwamuzi wa Gambia Bakary Papa Gassama alishinda tuzo ya mwamuzi bora kwa mara ya tatu mfululizo.

WASHINDI WA TUZO

Mchezaji bora wa Afrika wa mwaka
Riyad Mahrez (Algeria & Leicester City)

Mchezaji bora wa mwaka anayecheza Afrika
Denis Onyango (Uganda & Mamelodi Sundowns)

Mchezaji bora wakike wa mwaka
Asisat Oshoala (Nigeria & Arsenal)

Chipukizi mwenye kipaji cha aina yake
Kelechi Iheanacho (Nigeria & Manchester City)

Chipukizi bora wa mwaka
Alex Iwobi (Nigeria & Arsenal)

Kocha bora wa mwaka
Pitso Mosimane (Mamelodi Sundowns)

Klabu bora ya mwaka
Mamelodi Sundowns

Timu bora ya taifa ya mwaka
Uganda

Timu bora ya taifa ya wanawake
Nigeria

Mwamuzi bora wa mwaka:
Bakary Papa Gassama

Kikosi cha CAF cha wachezaji 11 wa 2016

Kipa: Denis Onyango (Uganda & Mamelodi Sundowns)

Mabeki: Serge Aurier (Cote d’Ivoire & PSG), Aymen Abdenour (Tunisia & Valencia), Eric Bailly (Ivory Coast & Manchester United) na Joyce Lomalisa (DRC &AS Vita).

Viungo: Khama Billiat (Zimbabwe & Mamelodi Sundowns), Rainford Kalaba (Zambia & TP Mazembe), Keegan Dolly (Afrika Kusini & Mamelodi Sundowns).

Washambuliaji: Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon & Borussia Dortmund), Sadio Mane (Senegal & Liverpool), Riyad Mahrez (Algeria & Leicester City).

Wachezaji wa akiba: Aymen Mathlouthi (Tunisia & Etoile du Sahel), Kalidou Koulibaly (Senegal & Napoli), Salif Coulibaly (Mali & TP Mazembe), Islam Slimani (Algeria & Leicester City), Mohamed Salah (Misri & Roma), Kelechi Iheanacho (Nigeria & Manchester City) na Alex Iwobi (Nigeria & Arsenal)

No comments:

Post a Comment