Tuesday, 10 January 2017

Simba yaifungisha virago Yanga Kombe la Mpinduzi, sasa kucheza na Azam FC IjumaaNa Mwandishi Wetu
SIMBA imefanikiwa kuifunga Yanga kwa penalti 4-2 katika mchezo wa Kombe la Kombela Mpinduzi na sasa itakwaana na Azam FC katika fainali itakayofanyika Ijumaa kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.


Azam ilitinga mapema fainali baada ya kuifunga Taifa Jang'ombe kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja huo katika majira ya saa 10 jioni.
 
Domayo alifunga bao hilo dakika ya 33 kwa shuti la umbali wa kama mita 19, baada ya kuwazidi mbinu viungo wa Taifa Jang’ombe, ambapo sasa watacheza na Simba katika mchezo utakaofanyika Ijumaa.

Hatua hiyo ya penalti ilifikiwa baada ya Simba na Yanga kutoka suluhu katika dakika 90 za kawaida katika mchezo huo wa nusu fainali uliohudhuriwa na umati wa watazamaji.


Penalti za Simba zilifungwa na Nahodha Jonas Mkude, kipa Daniel Agyei, Muzamiru Yassin na beki Mkongo Janvier Besala Bokungu, wakati kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ alikosa penalti yake huku akifanikiwa kuokoa shuti la Mzimbabwe Method Mwanjali.

Waliofunga penalti kwa upande wa Yanga ni pamoja na Simon Msuva na kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko wakati kipa Mghana wa Simba, Daniel Agyei aliokoa penalti za Dida na Mwinyi Hajji Mngwali.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na waamuzi wa Zanzibar, Mfaume Ali Nassor, aliyesaidiwa na washika vibendera Mgaza Ally na Mbaraka Haule, Waziri Sheha mezani chini ya usimamizi  wa Ramadhan Nassor, ambapo timu zote zilishambuliana kwa zamu.

Pamoja na kuonekana kuingia uwanjani, kinyonge baada ya kufungwa 4-0 na Azam FC Jumamosi katika mchezo wa mwisho wa kundi A,  Yanga ilifanikiwa kuwazidi Simba katika dakika 45 za mwanzo.

Yanga tena wakalijaribu lango la Simba dakika ya 15, baada ya winga Simon Msuva kupiga mpira uliorudi kufuatia pigo la mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe kuokolewa, lakini kipa Agyei akaokoa tena akishirikiana na beki Method Mwanjali.

Simba wakajibu dakika ya 16 baada ya kiungo Mohammed Ibrahim kupiga shuti kali lililodakwa na kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’.

Msuva tena akakaribia kufunga dakika ya 36 baada ya kumtoka kwa chenga nzuri beki wa kulia wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na kumlamba chenga ya mpira wa kichwa kipa Agyei, lakini alipobinuka ‘kibaiskeli’ kwa pigo dhaifu lililokuwa linaelekea nyavuni, beki Janvier Besala  Bokungu akatokea na kuokoa.

 Vikosi vilivyoanza:


Yanga; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondan, Saidi Juma ‘Makapu’, Simoni Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Haruna Niyonzima na Deusi Kaseke.
Simba: Daniel  Agyei, Janvier Bokungu, MOhammed Hussein 'Tshabalala', Abdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, James Kotei, Juma Luizio, Muzamil Yassin na Mohamed Ibrahim.

No comments:

Post a Comment