Friday, 6 January 2017

Azam FC ikizubaa tu kwa Yanga imekula kwao njia nyeupe kupanda boti kurudi Chamazi kujiandaa na Ligi Kuu BaraNa Mwandishi Wetu, Zanzibar
MABINGWA wa soka Afrika Mashariki Azam FC ya Tanzania Bara italazimika kuifunga Yanga ili kutinga nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kutoka suluhu na Jamhuri juzi.

Azam FC ilijikuta ikiambulia pointi moja baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Jamhuri ya Pemba katika moja ya mechi za mashindano hayo kwenye Uwanja wa Amaan hapa.

Wakati Azam wakisubiri `huruma’ ya Yanga, mabingwa hao wa Tanzania Bara (Yanga), wenyewe tayari wameshakata tiketi ya kucheza nusu fainali baada ya juzi kuifunga Zima Moto kwa mabao 2-0.

Kimsimamo, Yanga wana pointi sita baada ya kushinda mechi mbili wakati Azam wenyewe mkononi wanashikilia jumla ya pointi mbili tu.

Nahodha wa Azam FC, John Bocco alisema baada ya mchezo huo dhidi ya Jamhuri kuwa, Yanga ni timu kubwa na wana kazi ngumu watakapokutana nao kesho kwenye Uwanja wa Amaan.

Endapo Azam FC itashindwa kuifunga Yanga itakuwa katika hali tete ya kucheza nusu fainali ya mashindano hayo na huenda ikapanda boti na kurejea jijini Dar es Salaam kuendelea na maandalizi ya Ligi Kuu Bara iliyosimama kwa muda kupisha mashindano hayo.

“Tunawaheshimu Yanga kwa kuwa ni timu kubwa. Tunajua nasi ni timu kubwa na bora, itakuwa mechi ngumu sana.

“Lakini tunaiweka kando mechi ya leo na tunaanza maandalizi kwa ajili ya mechi ijayo kujiandaa dhidi ya Yanga,” alisema.

Jamhuri ilichapwa mabao 6-0 na Yanga, hivyo kuondoka na pointi moja mbele ya Azam hakuna shaka kuwa matokeo hayo yatakuwa ni faraja kubwa sana kwao.

Pambano hilo la Yanga na Azam FC litafanyika kwenye Uwanja wa Amaan kuanzia 2:30 usiku.

No comments:

Post a Comment