Monday 23 January 2017

Wenger kikaangoni FA yampa hadi alhamisi kujibu mashtaka yanayomkabili


Mwamuzi wa akiba, Anthony Taylor (kushoto) akimtaka kocha wa Arsenal, Arsene Wenger kutoka baada ya kutolewa uwanjani na mwamuzi Jonathan Moss (hayuko pichani) wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Burnley kwenye Uwanja wa Emirates Stadium jijini London mwishoni mwa wiki.
 

LONDON, England
KOCHA Mkuu wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger ameshtakiwa na Chama cha Soka (FA) kwa madai ya kutoa lugha chafu na kumsukuma mwamuzi wa akiba wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Burnley.

Wenger alimsukuma mwamuzi msaidizi, Anthony Taylor baada ya kutolewa nje katika mchezo huo,a mbao uliofanyika Jumapili na Arsenal kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Kocha huyo alijikuta akitolewa nje baada ya kufoka katika dakika ya 93 kufuatia penalti waliyopewa Burnley, ambao walikuwa nyuma kwa bao 1-0.

Katika mchezo huo, Burnley walifikiri kuwa kwa mara ya pili wangeweza kuondoka na pointi moja ugenini msimu huu baada ya Andre Gray kufunga bao la kusawzisha kwa penalti baada ya Francis Coquelin akiadhibiwa kwa kumchezea vibaya Ashley Barnes.

Hatahivyo, the Gunners ndio walikuwa wa kwanza kupata bao baada ya Shkodran Mustafi kufunga bao la kuongoza katika kipindi cha pili akiunganisha wavuni mpira wa kona iliyochongwa na Mesut Ozil akifunga bao lake la kwanza katika soka la Uingereza.

Alexis Sanchez ndiye aliyekuwa mkombozi wa Arsenal katika mchezo huo baada ya kuudokoa mpira katika dakika ya 98 na kumpita Tom Heaton baada ya Ben Mee kupigiwa filimbi kufuatia kumrushia daruga Laurent Koscielny, ambaye alionekana akiwa katika nafasi ya kuotea.

Kwa upande wa Wenger, 67, kocha huyo mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo aliomba radhi na amepewa hadi Alhamisi awe amejibu tuhuma hizo.

Taarifa ya FA ilisomeka: "Inadaiwa kuwa katika dakika ya 92, Wenger alitumia lugha chafu au za kukera dhidi ya mwamuzi wa akiba.

"Inadaiwa zaidi kuwa kufuatia kutolewa nje kutoka eneo la ufundi, kocha huyo aliendeleza ujeuri katika njie ya kuingilia katika vyumba vya kubadiishia nguo baada ya kumsukuma mwamuzi msaidizi…”

Baada ya kutakiwa na mwamuzi Jon Moss kwenda kukaa jukwaani, Wenger aliondoka kutoka uwanjani lakini alisimama kati njia ya kuingilia na kugoma kutoka akijaribu kuangalia sehemu iliyobaki ya mchezo kutoka hapo, ambapo Taylor alijaribu kumshawishi kuondoka lakini badala yake alimsukuma mwamuzi huyo msaidizi.

No comments:

Post a Comment