Tuesday 31 January 2017

Mkwasa atangazwa rasmi leo kuwa Katibu Mkuu mpya wa Yanga Africans



Na Mwandishi Wetu
MCHEZAJI na kocha wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Charles Boniface Mkwasa (Pichani) leo ametambulishwa rasmi kuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, akichukua nafasi ya Baraka Deusdedit anayerejea kwenye Idara yake ya Fedha.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo katika Makao Makuu ya klabu hiyo, Jangwani, Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema kwamba Mkwasa anaanza majukumu yake rasmi Februari 1, mwaka huu.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga akizungumza leo na waandishi wa habari.
Sanga alisema kuwa sababu kubwa ya kumchagua Mkwasa ni kuhimarisha safu ya uongozi wa klabu hiyo  ambapo aliyekuwa kaimu katibu mkuu, Baraka Deusdedit anarejea katika nafasi yake ya zamani ya Ukurugenzi wa Fedha.“Najua wadau wa soka wanajiuliza kwa nini Mkwasa ameshika nafasi hiyo ya Ukatibu Mkuu kwa sabab ya taaluma yake inayojulikana ni ufundisha mpira wa miguu, siyo kweli, Mkwasa anauzoefu mkubwa katika kazi hiyo tofauti na watu wanavyomuelewa,”

“Na hii si mara ya kwanza, hata Zambia, Kalusha Bwalya amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka nchini humu huku wakijua kuwa ni mchezaji mstaafu au kocha, Yanga tumemuona Mkwasa ni bora katika nafasi hiyo,” alisema Sanga.
 
Mkwasa alishukuru kushika nafasi hiyo na kuahidi kuifikisha Yanga katika malengo yaliyowekwa. “Naomba nieleweke wazi kuwa mimi ni Katibu Mkuu wa Yanga na wala siyo kocha, najua kuna watu watafikiria kuwa narejea kwa mlango wa nyuma, kamwe sitaingilia masuala yoyote ya ufundi zaidi ya kufanya yale yaliyomo katika majukumu yangu,” alisema Mkwasa.

“Ninaomba ushirikiano kutoka kwa wanachama, mashabiki, viongozi wenzangu, sisi sote tupo hapa Yanga kwa ajili ya kuiletea maendeleo na si vinginevyo,” alisema.

Mkwasa anarejea Yanga ndani ya mwezi mmoja tangu aondolewe timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na nafasi yake kupewa Salum Mayanga.

Mkwasa aliifundisha Taifa Stars tangu Julai mwaka 2015 baada ya kurithi nafasi ya Mholanzi, Mart Nooij na katika kipindi chake aliiongoza timu hiyo katika mechi 13 za kimatafa, ikishinda mbili, kufungwa sita na sare tano.

No comments:

Post a Comment