Monday 25 September 2017

Wagombea Chaneta kupiga kampeni kiduchu

Annie Kibira

Na Mwandishi Wetu

WAGOMBEA watakaopitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) Jumamosi mjini Dodoma, watakuwa na muda mfupi wa kujinadi.

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi huo iliyotolewa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni Alhamisi wakati usaili utafanyika Ijumaa na uchaguzi Jumamosi.

Mwenyekiti wa Chaneta, Annie Kibira amesema leo kuwa muda wa kampeni ni mdogo sana, lakini itabidi kufuata utaratibu uliowekwa na BMT, ambao ndio wasimamizi wa uchaguzi huo.

Alisema hawaruhusiwi kufanya kampeni hadi baada ya usaili kwani kutofuata utaratibu huo, unaweza kukatwa kwani utakuwa umekiuka utaratibu.

Halima Bushiri;Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Naye Ofisa Michezo wa BMT, Halima Bushiriki amesema leo kuwa wamepanga ratiba hiyo ili kuwaepuesha wagombea na wapiga kura kuingia gharama.

Alisema hadi jana wagombea 14 wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali walirudisha fomu kati ya 25 waliochukua fomu hizo, huku akiwasisitizia watu kuendelea kuchukua na kurudisha kwa wakati ili kufanikisha zoezi hilo.

Pia aliwataka wadau mbalimbali wa michezo bila kujali jinsi, yaani wanawake na wanaume wenye sifa  kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu hizo ili kugombea uongozi.

Aliwataja waliorudisha hadi jana kuwa ni Annie Kibira (uenyekiti), Dk Devota Muro, Luiza Jellah (ujumbe), Mwajuma Kisengo (katibu msaidizi/mjumbe), Asha Sapi (ujumbe) na Winfrida Emmanuel (makamu mwenyekiti),

Wengine waliorejesha fomu ni Hilda Mwakatobe (katibu msaidizi), Judith Ilunda (katibu mkuu/ujumbe), Zakia Kondo (ujumbe), Julieth Mndeme (ujumbe), Pili Mongella (makamu mwenyekiti/ujumbe).

No comments:

Post a Comment