Wednesday 13 September 2017

Uhamiaji netiboli yaanza vizuri kutetea taji Ligi Daraja la Kwanza kwa kuifunga Polisi Moro 37-34

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya netiboli ya Uhamiaji imeanza vizuri kampeni zake ya kutetea taji la Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara baada ya kuifunga Polisi Morogoro 37-34 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika mjini Moshi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) Annie Kibira, Polisi Morogoro ilikuwa mbele kwa mabao 21-17 na kuonekana kama ingeibuka na ushindi katika mchezo huo kabla ya mambo kuwageukia kipindi cha pili.

Naye kocha wa Uhamiaji, Winnie Emmanuel alisema kuwa mashindano ni magumu lakini wamejiandaa kuhakikisha wanatetea taji lao vizuri.

Emmanuel aliwataka wapenzi wa michezo wafike kwa wingi kushuhudia uhondo kutoka kwa Uhamiaji ambayo imejiandaa vizuri kulitetea taji lao walilolitwaa mwaka jana.

Hatahivyo, alisema kuwa kuna sababu kadhaa zilizoifanya timu yake kushindwa kuibuka na ushindi mnono, ikiwemo hali ya hewa, kubaki nyuma kwa baadhi ya wachezaji wao kwa sababu ya majukumu ya kikazi.
Annie Kibira.
Alisema kuwa wachezaji hao wanatarajia kuwasili kesho mjini Moshi, ambapo anatarajia watakiongezea nguu kikosi chao katika mashindano hayo.

Uhamiaji kesho itacheza dhidi ya Madini ya Arusha huku ndugu wawili, Polisi Moro watashuka dimbani kucheza dhidi ya Polisi Arusha.

Mechi zingine za kesho ni pamoja na Polisi Arusha itakayopepetana na Jeshi Stars wakati Arusha Queens itacheza dhidi ya dada zao wa Madini, JKT Mbweni watacheza na Tanga Jiji.


Polisi Morogoro itacheza na Madini katika moja ya mechi za jioni zitakazofanyika wakati wa ufunguzi rasmi wa mashindano hayo.

No comments:

Post a Comment