Thursday 7 September 2017

Okwi, Murshid watua kuiongezea Simba nguvu


Na Mwandishi Wetu
NYOTA wa kimataifa wa Simba waliokuwa na kikosi cha timu ya taifa ya Uganda, The Cranes, beki Juuko Murshid na mshambuliaji, Emannuel Okwi wanatarajiwa kutua jana jijini Dar es Salaam tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC utakaofanyika jesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Akizungmza Waandishi wa Habari kweye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Haji Manara amesema kwamba Juuko na Okwi walitarajia kutua jana na kujiunga na wenzao kambini kwa ajili ya mchezo huo.

“Akina Okwi tunawatarajia kufika leo (jana)  kutoka Uganda na watajiunga moja kwa moja na wenzao kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Jumamosi dhidi ya Azam,” amesema Manara.

Ofisa huyo wa Simba amesema mchezo huo utakuwa mgumu kwa sababu Azam ni timu nzuri na wao wamejipanga vizuri ingawa bado wana majeruhi wawili tu, kipa Said Mohammed ‘Nduda’ na beki Shomari Kapombe.

Manara amesema kwamba Kapombe ataanza mazoezi Jumatatu wakati Nduda ataondoka wikiendi hii kwenda India kwa ajili ya upasuaji wa goti.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Iddi Maganga amesema kwamba kikosi chao kinaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo huo na watajitahidi kuvuna pointi tatu ili kuonyesha thamani ya kucheza nyumbani.

“Tunawaheshimu wapinzani wetu, Simba ni timu nzuri na tunatarajia mchezo utakuwa mgumu, lakini tunaamini pia ubora wa kikosi chetu na maandalizi ni silaha yetu nzuri ya ushindi siku hiyo,”amesema Maganga. 

Mapema katika Mkutano huo, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema kwamba mchezo huo utachezeshwa na refa Ludovick Charles wa Tabora, atakayesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza na Abdallah Mkomwa wa Pwani na mezani atakuwepo Josephat Bulali na Kamisaa  atakuwa Ruvu Kiwanga, wote wa Dar es salaam.

Ikumbukwe viingilio katika mchezo huo utakaoanza Saa 1:00 usiku vitakuwa ni Sh. 10,000 kwa jukwaa la VIP na 7,000 kwa mzunguko.

No comments:

Post a Comment