Tuesday, 19 September 2017

Tetemeko la Ardhi laua Watu 140 nchini Mexico

MEXICO CITY, Mexico

TETEMEKO kubwa la ardhi limeikumba Mexico na kupoteza maisha ya zaidi ya watu 140 na kuharibu majengo mengi katika jiji hili, imeelezwa.

Angalau watoto 21 wanahofiwa kufa na wengine wakiripotiwa kupotea baada ya shule kuanguka katika jiji hilo.

Tetemeko hilo linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa magnitude 7.1 pia limesababisha uharibifu mkubwa katika nchi za jirani.

Kwa mara ya mwisho tetemeko kubwa kama hilo liliwahi kutokea takribani miaka 32 iliyopita baada ya tetemeko kuua maelfu ya watu Mexico City.

Hilo ni tetemeko la pili kutokea baada ya lile la mapema mwezi huu ambalo lilikuwa na ukubwa na magnitude 8.1 ambalo liliua watu 90 lilitokea kusini mwa nchi hii.

Angalau watu 149 wamekufa nchi nzima, kimeeleza chanzo kimoja cha habari.

Angalau watu 55 wamekufa katika Jimbo la Morelose,kusini mwa Mexico City, huku 32 wakifa huko Pueblae. Watu 49 wanahofiwa kupoteza maisha Mexico City, huku wengine 10 wakifa katika Jimbo la Mexico, na watau wakifa huko Guerrero.

Karibu watu milioni 2 wakazi wa Mexico City wameachwa bila ya umeme huku nyaya za simu zikiwa zimeanguka. Wananchi wameonywa kutovuta sigara mitaani kwani gesi inaweza kulipuka.

Meya wa Mexico City Miguel Angel Mancera aliaimbia TV moja kuwa huduma za uokoaji zinaendelea kuchimba katika makazi 44 ili kuona kama kuna watu wamefukiwa na kifusi.

Kaimu Katibu wa Elimu Javier Treviño, alikaririwa na vyombo vya habari vya haba kuwa, watoto 21 na watu wazima wanne walikufa wakati shule ya Enrique Rebsamen iliyopo kusini mwa Mexico City ilipoanguka.

Baadhi ya wanafunzi waliokolewa, vyombo vya habari vya Mexico viliripoti, lakini wengine bado hawajapatikana.

Nyumba za gholofa, maduka makubwa na kiwanda navyo pia ni baadhi ya vitu vilivyoanguka jijini hapa.

Akihutubia kupia televisheni, Rais wa Mexico Peña Nieto alisema dharura imechukulia katika maeneo yaliyoathirika na jeshi limekwenda kutoa msaada.

Karibu sehemu zote katika jiji la Mexico, timu ya watu wa uokoaji na wake wakujitolea wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali kuwaokoa watu.

"Mke wangu yuko pale. Sijaweza kuwasiliana naye, “alisema Juan Jesus Garcia, 33, huku akitokwa na machozi jirani na jengo lililoanguka.

"Hajaweza kujibu simu na sasa tumeambia kuzima simu zetu za viganjani kwa sababu kuna gesi inayovuja inaweza kulipuka.”

Tetemeko hilo la ardhi limetokea  jijini Mexico wakati wa kumbukumbu ya miaka 32 ya tetemeko jingine la ardhi lililoua watu 10,000.


Mexico City ni moja ya majiji yenye watu wengi duniani, ambapo ina zaidi ya wakazi milioni 20 wanaoshi hapo.

No comments:

Post a Comment