Tuesday 12 September 2017

Mourinho ailaumu Man United licha ya kushinda 3-0

LONDON, England

KOCHA Jose Mourinho ameweka matumaini ya Manchester United kufanya vizuri katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya kuikosoa timu yake `kubweteka’ katika mchezo huo ambao wameshinda 3-0 dhidi ya Basle.

Marouane Fellaini, Romelu Lukaku na Marcus Rashford wote walifunga mabao yao ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya wakati Man United ikishinda kwa urahisi katika mchezo huo dhidi ya timu hiyo ya Uswisi uliofanyika kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Mourinho, anasaka kushinda taji la mashindano hayo kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo akiwa na Porto na Inter Milan, aliwatuhumu wachezaji wake kubweteka baada ya bao la Lukaku lililoifanya timu hiyo kuwa mbele kwa mabao 2-0 muda mfupi baada ya mapumziko baada ya kutawala kipindi cha kwanza.

"Pointi tatu ni muhimu sana wakati unaoanza hatua ya makundi kwenye uwanja wa nyumbani, “alisema Mourinho, ambaye aliiwezesha United kutwaa taji la Ligi ndogo ya Europa msimu uliopita wakati wa shindano lake la kwanza Ulaya tangu aanze kuifundisha timu hiyo msimu uliopita.

"Hadi 2-0 tulikuwa vizuri, tukijiamini na kucheza kwa utulivu, tulifanya maamuzi mazuri, kiujumla tulicheza vizuri.

"Baada ya hapo kila kitu kilibadilika. Tuliacha kufikiri, tuliacha kucheza vizuri, tuliacha kufanya maamuzi sahihi uwanjani na kusababisha kujiweka matatani.”

Basle walipata baadhi ya nafasi nzuri lakini hawakuwa tishio kuwaadhibu Man United katika kipindi cha pili.

Hatahivyo, Mourinho alijua kuwa aina hiyo ya makosa ingeweza kukiadhibu kikosi chake.


Katika mchezo huo Man United walipata pigo baada ya mchezaji wake Paul Pogba, kutolewa nje baada ya kuumia katikati ya kipindi cha kwanza.

No comments:

Post a Comment