Monday, 25 September 2017

LONDON, England

TIMU ya Brighton imeichapa Newcastle United bao 1-0 na kupata ushindi wa pili mfululizo katika mechi za Ligi Kuu ya England.

Wenyeji walipata bao wakati krosi ya Pascal Gross iliporejeshwa nyuma kwa kichwa na Dale Stephens na Tomer Hemed alifunga kutoka umbali wa meta sita.

Newcastle, ambayo ilishinda mechi zake tatu zilizopita, ilikuwa na nafasi, lakini mpira wa Mikel Merino ulipanguliwa na Mat Ryan, huku Joselu mara mbili akishindwa kufunga na mchezaji aliyetokea benchi Jonjo Shelvey, shuti lake likigonga mwamba.

Ushindi huo umeiwezesha Seagulls kupaa hadi nafasi ya 13 katika msimamo, wakati Newcastle imeporomoka hadi nafasi ya tisa.

Newcastle ilitawala zaidi mchezo huo na kupiga mashuti mengi lakini kikosi hicho kinachofundishwa na Rafael Benitez, kilishindwa kulazimisha sare.

Wachezaji waliongia wakitokea benchi Jesus Gamez na Dwight Gayle jitihada zao za dakika za mwisho zilishindwa kuzaa matunda, ambapo mashuti yao yaliokolewa na Ryan.

No comments:

Post a Comment