Sunday 17 September 2017

KMC yaanza vizuri LIgi Daraja la Kwanza Bara

Kocha wa KMC, Felix Minziro.
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya soka ya Mawenzi Market ya Manispaa ya Morogoro inayoshiriki kwa mara ya kwanza Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara imeshindwa kutamba katika uwanja wake wa nyumbani baaada ya kufungwa na KMC ya Kindondoni, Jijini Dar es Salaam kwa mabao 2-1.

Licha ya  kipindi cha pili Mbunge wa Jimbo la Morogoro mjini, Abdulaziz Abood kuwaahidi wachezaji donge nono la Sh 800,000 endapo wangeshinda mchezo huo huku ikiwa nyuma kwa  bao 1-0 hadi mapumziko ilishindwa kunyakua kitita hicho  kwa kupoteza mchezo huo kwenye uwanja wa nyumbani wa Jamhuri wa mjini Morogoro.

Bao la kwanza la Kinondoni ilipachikwa dakika ya nne na mchezaji wa zamani wa timu ya Yanga  Stephen Mwasika  na lilidumu hadi mapumziko, ambbapo  kipindi cha pili dakika ya 51 vijana wa Mawenzi Market walisawazisha bao hilo kupitia mchezaji Maulid Iddi kwa shuti hafifu baada ya mpira wa adhabu uliookolewa na beki wa Kinondoni kumkuta mfungaji.

Timu ya Kinondoni ambayo ilikuwa na baadhi ya wachezaji wenye uzoefu wa Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza ikiwa na  Kocha Mkuu , Fred Felix Minziro ‘ Majeshi’ ilibadili  mfumo wa uchezaji wa  pasi fupi na kutumia pasi ndefu uliowezesha kupata  bao la pili na  la ushindi katika dakika ya 86 kupitia Cliff Athony baada ya mpira uliopingwa na Mwasika kugonga mwamba na kumkuta mfungaji huyo.

Hadi dakika 90 za mchezo huo vijana wa  KMC kutoka Kinondoni  Jijini Dar es Salaam waliibuka kidedea kwa ushindi wa mabao  2 -1 dhidi ya  Mawenzi Market.

No comments:

Post a Comment