Tuesday 6 June 2017

Simba watolewa Kombe SportPesa Super Cup

Mwandishi Wetu
WAWAKILISHI wa Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Afrika, Simba (Pichani) wameyaaga mashindano ya SportPesa Super Cup baada ya kufungwa na timu isiyo na jina ya Nakuru All Stars ya Kenya kwa penalti 5-4.

Matokeo hayo ya kufungwa kwa Simba, sasa yanaifanya timu hiyo kuwakwepa watani zao wa jadi Yanga, ambayo juzi walitinga nusu fainali.

Yanga tayari jana walikaririwa wakisema kuwa wanataka kukutana na Simba katika fainali ya mashindano hayo ili kuisikisha adabu timu hiyo iliyomaliza ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka suluhu katika dakika 90 za kawaida na kumsaka mshindi kwa matuta ili kumpata mshindi.

Mchezaji aliyezamisha jahazi la Simba alikuwa kipa wa timu hiyo, Daniel Agyei baada ya kukosa penalti ya pili aliyoipiga na hivyo kutolewa kwa 5-4.

Hii ni mechi ya tatu kuamriwa kwa matuta baada ya ile ya Yanga kuitoa Tusker kwa penalti 4-2, huku Singida United nayo ikitolewa kwa penalti AFC Leopard kwa penalti 5-4 baada ya kutoka sare ya 1-1 katika dakika 90.

Kwa ushindi huo, Nakuru All Stars iliyopo katika ligi daraja la kwanza itacheza dhidi ya Wakenya wenzao, Gor Mahia katika mchezo wa nusu fainali utakaopigwa kesho Alhamisi.

Katika mchezo huo wa Simba na Nakuru, timu zote zilishambuliana kwa zamu na kukosa nafasi kadhaa za wazi hadi kufikia hatua ya kupigia penalti.

Katika mchezo wa kwanza jana kwenye Uwanja huo, Gor Mahia iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Jang’ombe Boys ya Zanzibar.

Mabao ya washindi katika mchezo huo yalifungwa na Middie Kagere katika dakika ya 63 na 83.
Wachezaji wa Simba waliopata penalti ni Mwinyi kazimoto, Hafidh Mussa, Feston Munezero na Jamvier Bukungu wakati Agyei alikosa.


Wakati penalti za Nakuru All Stars zilifungwa na Nganga Peter, Amakanji Japheth, Siwa Omond, Maina Geofrey na Nturukundo Jerome.

No comments:

Post a Comment