Friday 2 June 2017

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege waadhimisha Siku ya Mazingira kwa kufanya usafi Terminal Three leo

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),  Salim Msangi (kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa TAA, Mohamed Ally wakifanya usafi nje ya jengo la kuwasili na kuondokea abiria mashuhuri (VIP) leo wakati wafanyakazi wa mamlaka hiyo wakiadhimisha Siku ya Mazingira .
Na Mwandishi Wetu
MAKAO Makuu ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) itatoa tuzo kwa mameneja wote watakaofanya vizuri katika utunzaji wa mazingira.

Hayo yalisemwa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Salim Msangi wakati wafanyakazi wa mamlaka hiyo wakifanya usafi nje ya Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Dar es Salaam (JNIA) Terminal 3 kuadhimisha Siku ya Mazingira.
Siku ya Mazingira Duniani inafanyika kesho nchini Canada wakati kitaifa itafanyika mjini Butiama mkoani Mara, ambapo Makamu wa Rais Samia Hassan Suluhu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Msangi alisema kuwa, aliwataka mameneja wa viwanja vyote nchini kutunza mazingara, ambapo aliahidi kuwa atatoa tuzo kwa yule atakayefanya vizuri zaidi.
Fulana iliyobeba ujumbe wa Mazingira wa Mwaka huu.
Alisema kuwa wafanyakazi wa viwanja vya ndege wamekuwa mstari wa mbele kutunza mazingira miaka yote ili kuhakikisha jamii inaishi katika eneo salama.
Baadhi ya mabosi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakifanya usafi leo jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani wa mamlaka hiyo, Irene Sikumbili, mwanasheria wa TAA, Ramadhani Maleta na Mohamed Ally, Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu. 
 Mbali na kufanya usafi wa kufyeka nje ya Terminal 3, pia wafanyakazi hao wa TAA Makao Makuu, waliweka mbolea na kupalilia miti waliyopanda mwaka 2014 katika eneo la kufikia na kuondokea abiria la watu mashuhuri la VIP kwenye uwanja huo eneo la Terminal Two.

Kila mwaka wafanyakazi hao wa TAA wamekuwa wakifanya usafi au utunzaji wa mazingira katika maeneo tofauti tofauti.
Akifafanua kuhusu tuzo, Msangi alisema kuwa ataanzisha tuzo na atakayeshinda atapewa tuzo hiyo itakayoshindaniwa na viwanja vyote kupitia mameneja wao.

“Nitaanzisha tuzo na meneja atakayeshinda nitamzawadia na pamoja na wafankaazi wake ili kuhamasisha viwanja vingie nao wafanye vizuri ili washindi mwaka unaofuata, “alisema Msangi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Salim Msangi.
Pia alizitaja shughuli zingine wanazofanya ili kutunza mazingira ni pamoja na kudhibiti maji taka yanayotoka viwajani, ambapo wana mabwawa yanayokusanya maji yote, ambayo yanakuwa trited na kuwa safi kwa ajili ya matumizi mengine ya binadamu.
Alisema kuwa mbali na hiyo pia wana mfumo mwingine ambao hutenganisha maji na mafuta ili kulinda mazingira, ambapo usalama wa anga unachangia karibu asilimia mbili ya uchafuzi wa mazingira kutokana na ndege kutoa hewa ya ukaa.

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wakifanya usafi leo.

Mkuu wa Kitengo cha Mazingira wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Jofta Timanya akihojiwa na ITV leo.

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) baada ya kumaliza kufanya usafi leo nje ya jengo la Uwanja wa Kimataifa wa Ndege la Julius Nyerere (JNIA) Terminal Three leo.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, Salim Msangi (kulia) akizungumza na mwanasheria wa mamlaka hiyo, Ramadhani Maleta leo kabla ya kufanya usafi nje ya Jengo la kuwasili na kuondokea abiria mashuhuri, VIP, la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, JNIA, leo.


No comments:

Post a Comment