Tuesday, 6 June 2017

Gor Mahia yatinga nusu fainali SportPesa

Meddie Kagere (kushoto) wa Gor Mahia ya Kenya akipiga mpira pembeni ya beki wa Jang'ombe Boys ya Zanzibar, Ibrahim Said (kulia) katika mchezo wa SportPesa Super Cup uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.  Gor Mahia ilishinda 2-0.
Na Mwandishi Wetu
MICHUANO ya SportPesa imezidi kupamba moto baada ya timu ya Kenya ya Gor Mahia kutinga nusu fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Jang’ombe Boys ya Zanzibar katika mchezo uliofanyika mapema leo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Mabo yote mawili ya washindi yalifungwa na mshambuliaji wazamani wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu hizo zote zilikwenda mapumzikoni zikiwa suruhu kabla ya Gor Mahia kupata mabao yote mawili kupitia kwa mshambuliaji huyo aliyeitoa timu hiyo kimasomaso.

Mganda huyo aliyechagua kuchezea timu ya taifa ya Rwanda, alifunga bao la kwanza dakika ya 64 kwa kichwa akimalizia krosi ya Muguna Kenneth kabla ya kufunga la pili kwa penalti katika dakika ya 84, baada ya beki mmoja wa Jang’ombe Boys kuunawa mpira katika eneo la hatari.

Gor Mahia sasa itakutana na mshindi wa mchezo wa pili unaoanza hivi sasa, kati ya mabingwa wa Kombe la Shirikisho la Tanzania, Simba SC ya Dar es Salaam na Nakuru All Stars ya Kenya.


Mabingwa wa Tanzania Yanga tayari wametangulia kucheza nusu fainali baada ya jana kushinda kwa penalti 4-2 dhidi ya mabingwa wa Kenya, Tusker, ambao walitoka suluhu katika muda wa kawaida wa mchezo huo, huku AFC Leopards wakaitoa Singida United kwa penalti  5-4 baada ya sare ya 1-1.

No comments:

Post a Comment