Saturday, 3 June 2017

Real Madrid, Juventus fainali ya kufa mtu Ulaya leo

Kocha wa Juventus, Massimiliano Allegri.
CARDIFF, England
 FAINALI ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inachezwa leo jijini Cardiff ambapo Real Madrid inaumana na Juventus huku ikiwa ina nia ya kuweka historia ya kulichukua kombe hilo mara mbili mfululizo.

Read Madrid, mabingwa watetezi, ikitwaa kombe hilo itakuwa ya kwanza kulichukua mara mbili mfululizo lakini iko katika wakati mgumu kutimiza ndoto hiyo kutokana na ushindani wa Juventus inayong'arishwa na mshambuliaji Gonzalo Higuain.

Tangu kuanzishwa kwa Ligi hiyo mwaka 1993, hakuna iliyowahi kushinda kombe hilo mara mbili mfululizo zaidi ya AC Milan mwaka 1989 na 1990 lakini wakati huo lilikuwa likiitwa European Cup.
Mshambuliaji hatari wa Juventus ya Italia, Gonzalo Higuain.
Real Madrid chini ya Kocha Zinedine Zidane ilitwaa kombe hilo kwa mara ya 11 ilipoibuka na ushindi dhidi ya Atletico Madrid katika fainali ya msimu uliopita.
Kocha wa Real Madrid,  Zinedine Zidane.
Akizungumzia mchezo wa leo Zidane alisema kikosi chake kimejiandaa vema na wachezaji wana hali nzuri.

Alisema imewachukua muda na nguvu nyingi kujiandaa kufikia hatua hiyo muhimu na kuwa kwa sasa kilichobakia ni kuchukua ubingwa tu.

Juventus mara ya mwisho kushinda kombe hilo ilikuwa mwaka 2006 chini ya Kocha Marcello Lippi. Tangu hapo imefungwa mara nne hatua ya fainali ikiwa ni pamoja na ile ya mwaka juzi na Barcelona.
Real Madrid wakiwa mazoezini.
Juventus inayoshiriki Ligi Kuu Italia, ni timu ya tisa kushinda Ligi Kuu hiyo na Kombe la Ulaya na ni ya pili kufikia hatua hiyo tangu msimu wa mwaka 2009 na 2010, ambapo Inter Milan iliibuka mabingwa.

Kocha wa Juventus, Massimiliano Allegri alipoulizwa hatua hiyo ya kucheza fainali alisema kuwa hiyo ni hatua kubwa na ngumu kuifikia.

Alisema Juventus imeshapoteza fainali sita kati ya nane, ambazo timu yake imewahi kucheza Ulaya. Alisema kuna Ligi ya Mabingwa moja tu kwa Ulaya nzima na anaona kuwa amefikia hatua kubwa na ya muhimu zaidi kuongoza timu kucheza fainali hiyo. 

No comments:

Post a Comment