Saturday 24 June 2017

Umitashumta yaunda Kamati kubaini vijeba

Na Mwandishi Wetu, Mwanza
UONGOZI wa Mashindano ya Michezo ya Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) umeunda Kamati Maalumu kwaajili ya kudhibiti wanafunzi wenye umri mkubwa ambao wanashiriki katika mashindano hayo.

Akizungumza jijini hapa, Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Elimu, Jeshi Lupembe alisema wameunda kamati hizo ili kuondoa malalamiko yanayoletwa na walimu katika mashindano hayo.

Lupembe alisema kamati alizounda zina watalamu mbalimbali waliobobea katika michezo, ambao hadi sasa uongozi wao umetoa fomu maluumu kwaajili ya malalamiko yahusuyo wanafunzi waliozidi umri wanaoshiriki michezo hiyo.

Akielezea zaidi,Lupembe alisema mikoa inayotuhumiwa kuwa na wachezaji wenye umri mkubwa ni pamoja na Dar es Salaam, Tanga, Kigoma na Mara.

Lupembe alisema kamati yake kazi kubwa inayofanya ni kumhoji mtoto husika, kupeleleza mkoa alikotoka, shule, ofisa elimu, walimu na wazazi kuwahoji ili kujua  umri halali wa mtoto.

Kwa mujibu wa Jeshi, mpaka sasa waliotuhumiwa katika orodha ya watoto waliozidi umri ni 10 na  katika hao kuna watoto watatu wako vizuri, lakini saba waliobaki wameonywa kutoshiriki mashindano hayo.

Aidha, Mkurugenzi Lupembe alisema Serikali itaendelea na jitihada za mazungumzo ya kutafuta udhamini wa mashindano hayo kama ilivyo kwa Michezo ya Shule za Sekondari (Umisseta).


Katika mechi za leo mpira wa miguu kwa wavulana, Mwanza imeshinda 3-0 dhidi ya Manyara, Mpira wa mikono wasichana Mara imeshinda 13-9 dhidi ya Mtwara, Shinyanga 8-5 Dodoma na Mara 6-4 Dar-es-salaam.

No comments:

Post a Comment