Tuesday 25 August 2015

Polisi yampiga stop Lowassa kutembelea wananchi uswahilini



Waandishi Wetu
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limemuonya mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, kuwa staili ya kampeni aliyoianzisha ya kutembelea maeneo mbalimbali katika ziara zisizo rasmi, inahatarisha usalama wa raia na mali zao, hivyo iachwe.

Onyo hilo limewagusa pia wagombea wa vyama vya siasa katika nafasi mbalimbali hasa urais, ikielezwa kuwa, katika ziara hizo hujitokeza watu wengi, ambapo pia wahalifu wanaweza kutumia mwanya huo kufanya vitendo vya uhalifu.

Akizungumza na vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova alisema, baadhi ya wagombea wa vyama vya siasa wameanzisha mtindo wa kutembelea maeneo mbalimbali kama vituo vya daladala na masoko kwa madai ya kuyatembelea makundi ya watu wenye kipato cha chini.

Kamishna Kova alisema, kutokana na uzoefu uliojitokeza katika ziara hizo zisizo rasmi, imeonekana mikusanyiko mikubwa isiyotegemewa katika hali inayoashiria uvunjifu wa amani.

Kova alisema lengo la marufuku hiyo haliko kisiasa bali ni kwa ajili ya usalama wa wananchi wote, kwani wao wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria na si siasa.

Alitaja miongoni mwa wagombea hao ni mgombea wa nafasi ya Urais kupitia Chadema, Edward Lowassa pamoja na mgombea mwenza, Juma Duni Haji, ambaye jana alikuwa akifanya ziara yake katika eneo la Kariakoo, wilaya ya Ilala.

Alisema saa 6:00 mchana katika makutano ya mtaa wa Swahili na Uhuru, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya alilazimika kukutana ana kwa ana na Lowassa ili kumpa tahadhari ya kiusalama.

Mgombea huyo alikuwa amezungukwa na wapanda pikipiki wasiopungua 40 pamoja na magari mengi, hali ambayo ilileta msongamano katika eneo hilo.

Lazima ieleweke wazi kwamba moja ya kazi za Jeshi la Polisi ni kudhibiti makundi makubwa ya watu katika namna ambayo kiongozi yeyote wa aina ya wagombea urais anatakiwa kulindwa katika kipindi chote cha kampeni hadi siku ya uchaguzi, alisema Kova.
Alisema ni vyema wagombea mbalimbali hasa wa urais waoneshe ushirikiano wa hali ya juu kwa Jeshi la Polisi ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza dhidi yao au kwa watu wengine.

Alisema jambo hilo linaweza kuonekana ni kawaida lakini yakitokea madhara lawama zote zitaenda kwa polisi kwa kushindwa kufanya kazi yao.

Hata hivyo, alisema marufuku hiyo ni kwa vyama vyote vyenye wagombea wanaoshiriki katika uchaguzi mkuu na kwamba atakayeamua kukaidi agizo hilo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Kamanda Kova alishauri viongozi wa vyama pamoja na wagombea wao kufuata ratiba za kampeni za mgombea urais na mgombea mwenza kwa vyama vya siasa kama ilivyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kuondoa hisia za kufanyika kampeni nje ya ratiba.

No comments:

Post a Comment