Saturday, 8 August 2015

RISALA YA MGENI RASMI WAKATI WA KUFUNGA MAFUNZO YA WALIMU MCHEZO WA MPIRA WA MIKONO, MKUZA, KIBAHA TANZANIA 07/08/2015.Washiriki wa mafunzo ya ufundishaji mpira wa mikono wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi pamoja na viongozi waliosimamia mafunzo hayo yaliyofanyika katika shule za Filbert Bayi Mkuza Kibaha jana Ijumaa.
 Katibu Mkuu, Kamati ya Olimpiki Tanzania  Ndugu Filbert Bayi

Viongozi wa Vyama vya Michezo (TAHA/ZAHA)

Mkufunzi wa Kimataifa,

Waratibu wa Mafunzo (TOC na TAHA/ZAHA)

Washiriki wa Mafunzo,

Mabibi na Mabwana.

Napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru TOC na TAHA/ZAHA kwa kunipa heshima hii ya kuwa mgeni rasmi katika kufunga mafunzo haya ya walimu wa mchezo wa Mpira wa Mikono.

 

Mafunzo haya ambayo yalifunguliwa siku 12 zilizopita na Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Ndugu Gulam Rashid ambaye nina uhakika amewaambia mambo mengi mazuri ambayo mnatakiwa kuyazingatia wakati wa mafunzo haya yaliyohusisha walimu na wachezaji wa Taifa.
Ni matumaini yangu kuwa mmepata dozi nzuri ya taaluma na mbinu mbalimbali ya kufundisha mchezo huu. TOC inauthamini sana  mchezo wa mpira wa mikono, kwani ni kati ya michezo ambayo TOC inaamini kuwa ni baadhi ya michezo iliyokuwa inapendwa sana na watanzania pamoja na kuchezwa katika Mikoa michache hasa na vilabu vya Majeshi yetu (Polisi, JWTZ, Magereza, JKT/JKU nk.

Kama kweli tunataka mchezo huu uenee nchi nzima, vyama husika havina budi kufanya jitihada ya kufufua vyama vya mchezo huu Mikoani kama vipo na kuanzisha katika  Mikoa ambayo havina vyama hivyo, hali kadhalika na kuueneza katika Shule zetu za Msingi na Sekondari ambapo ndipo penye vipaji vingi. Tusisubiri tu wakati wa Michezo ya Umisseta na Umitashumta Taifa.  

Kama nilivyofahamishwa vyema haya ni mafunzo ya pili kufanyika kwa walimu wetu hapa Tanzania. Mafunzo ya awali kwa walimu yalifanyika mjini Dar Es Salaam  mwaka 2007 yote yakifadhiliwa na  Olimpiki Solidariti kupitia Kamati ya Olimpiki Tanzania.

Pia naamini mmefaidika na elimu mliopata kutoka kwa mtaalamu wa Kimataifa Ndugu Tuma ambaye amekuwa wakiwaandalia masomo yote ya nadharia na vitendo kwa muda wote wa siku 11. Ni mategemeo yangu elimu mliyopata itawasaidia kuandaa timu zenu na kutambua vipaji vipya katika maeneo mnayotoka. Ni ukweli usiopingika kwamba  mmejiongezea elimu ya kufundisha mchezo huu wa mpira wa mikono kwa kiwango cha hali ya juu, mkilinganisha uwezo na elimu mliyokuwa nayo awali na wachezaji wa taifa kufaidika kwa ushiriki wao wa mara ya kwanza.
Wakati wote nimewahi kusikia TOC kuwa mstari wa mbele katika kuendeleza taaluma ya ufundishaji na mbinu za kisasa za kuboresha uwezo wa walimu, ili waweze kufikia viwango vinavyotakiwa kwa timu zetu zinaposhindana katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa.

Ningependa kusisitizia sana kwenu walimu mnaomaliza mafunzo haya kwamba, mhakikishe mchezo huu wa mipra wa mikono  unapiga hatua kufikia kiwango ambacho kitatupeleka kwenye michezo ya Kanda, Afrika na Kimataifa.
Tanzania haina tofauti na nchi kama Misri, Algeria, Nigeria, Tunisia nk  ambao zimekuwa tishio katika mchezo wa mpira wa mikono katika bara letu la Afrika.

Ningependa kuwasihi walimu mnaomaliza mafunzo haya leo kuupeleka mchezo huu mashuleni walipo vijana wengi wenye vipaji vingi ambao wanafundishika na rahisi kuelewa. Inahitajika mipango mahususi ya mazoezi na mashindano ambayo nina imani Vyama vyetu vya Mpira wa Mikono Tanzania Bara na Zanzibar wanayo mipango hiyo.

Wizara zinazoshughulikia michezo Tanzania zimetayarisha mipango kwa kushirikiana na vyama vya michezo kuendeleza michezo ya aina yote. Linalotakiwa hivi sasa ni kwa walimu wetu kutumia mafunzo haya katika kuendeleza mchezo wa mpira wa mikono nchini. Changamoto itoke kwenu ili Vyama, Mabaraza na Wizara husika na wanamichezo baadhi yao ambao wako hapa leo waweze kuchangamkia mipango yenu mtakayoandaa.
Napenda nichukue nafasi hii kumpongeza na kumshukuru mtaalamu wa Kimatafa Ndugu Tuma kwa jitihada zake za kutoa mafunzo haya kwa ufanisi mkubwa, waratibu wa TAHA/ZAHA, TOC na Walimu washiriki kwani bila wao kuwepo hapa mafunzo haya yasingefanyika.

Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru Olimpiki Solidariti kwa kufadhili mafunzo haya, Shirikisho la Kimataifa la mpira wa mikono (IHF) kwa kumteua  Mkufunzi niliyemtaja hapo juu kuendesha mafunzo, TOC na TAHA/ZAHA kwa maandalizi mazuri, mwisho kabisa nawashukuru wale wote waliohusika katika kufanikisha mafunzo haya kwa namna moja au nyingine hasa waratibu wa TOC na TAHA/ZAHA, Taasisi ya Filbert Bayi kama mwenyeji kwa huduma zote  nzuri mpaka kufika siku hii ya mwisho.
Kwa haya machache sasa natamka kwamba mafunzo yenu ya ualimu wa mchezo wa Mpira wa Mikono ninayafunga rasmi.


Ahsanteni!

No comments:

Post a Comment