Friday 14 August 2015

Azam TV yazindua channel ya michezo mitupu


Mratibu wa uzinduzi wa Channel ya Michezo ya Azam TV, F. Kaijage wakati wa uzinduzi huo leo.

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Azam Media imezindua chaneli mpya ya ‘Azam Sports HD’ itakayojihusisha na matangazo ya michezo.

Kuzinduliwa kwa chaneli hiyo ni moja ya mpango wa kampuni ya Azam media kujikita katika utoaji wa burudani kwa wapenzi wa michezo mbalimbali na wateja wa kampuni hiyo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa chaneli hiyo, Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Rhys Torrington alisema kuwa wateja wote wanaotumia huduma za televisheni ya Azam na waliolipia moja ya vifurushi vya king'amuzi watapata huduma hiyo kwa kuongeza malipo ya Sh. 15,000.

Naibu Mtendaji wa kampuni hiyo, Tido Mhando.
“Uzinduzi wa huduma yetu mpya ya chaneli ya Azam Sports HD ni hatua mojawapo ya mikakati yetu ya kuwapatia wateja wetu burudani ya michezo, "alisema.
 
Kila mtu anayetumia huduma zetu atapata fursa ya kuangalia michezo yote inayofanyika duniani,” alisema Torrington.
 
Alisema huduma hii ni ya wateja wote wanaopatikana Tanzania na kwa watumiaji wengine waliopo nje ya Tanzania hawataweza kuipata hadi hapo baadae.

Torrington alisema chaneli hii kwa kuanza itaonesha moja kwa moja mashindano ya mpira wa miguu wa kombe la La Liga na VPL ambapo inatarajiwa kuanza Agosti 21 mwaka huu kwa kuonesha pambano la mpira wa miguu katika ya timu ya Malaga na Seville.

Kwa upande wake Naibu Mtendaji wa kampuni hiyo, Tido Mhando alisema kuwa pamoja na kuonesha mechi mbalimbali za mpira wa miguu, chaneli hiyo pia itaonesha aina zingine za michezo kama vile mpira wa kikapu, mashindano ya magari na kuogelea.

“Tumeazimia kuwa watoa burudani wa uhakika kwa wateja wetu kwa kuwaletea karibu michezo yote waipendayo kupitia chaneli yetu hii mpya tuliyoizindua leo. Tutaanzia hapa nyumbani kwa kuonesha mapambano mbalimbali hadi Ulaya na mabara mengine,” alisema Mhando.
Mhando alisema kuwa chaneli hiyo itaongozwa na watangazaji mahiri na wenye uzoefu wa kutosha katika fani ya utangazaji wa michezo akiwemo Charles Hillary na wengine, hivyo wananchi watarajie kupata burudani ya uhakika.
 
Aidha, Mhando alisema chaneli hiyo itakuwa na vipindi vya uchambuzi wa kina wa michezo utakaoongozwa na wachambuzi waliogombea katika kazi hiyo ikiwemo Ally Mayay Tembele, Hussein Sappy, pamoja na Eddo Kumwembe.

No comments:

Post a Comment