 |
Bi. Delfine Mulogo wakati wa uhai wake. |
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),
inamlilia kwa masikitiko makubwa Mwanasheria wake Bi. Delfine Mulogo
(32) aliyekuwa Kituo cha kazi cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius
Nyerere (JNIA) aliyefariki dunia Desemba 25.
Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi, Bw.
Mtengela Hanga akisoma wasifu wa marehemu katika kanisa Katoliki Parokia ya
Mtakatifu Augustine Mbezi Temboni, alisema, atakumbukwa kwa uchapakazi, uhodari
na uadilifu wake kazini.
 |
Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya
Mtakatifu Augustine, Padri Fidelis Mfaranyembo lililopo Mbezi Temboni jijini
Dar es Salaam, akinyunyizia maji ya baraka kwenye mwili wa aliyekuwa
Mwanasheria wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Kituo cha Kiwanja
cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bi. Delfine Mulogo
kabla ya kusafirishwa kwenda Kijiji cha Uru Kishumundu Mkoani Kilimanjaro kwa
maziko.
|
“Tunasikitika kumpoteza mwanasheria huyu kijana,
kwa niaba ya Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, tunatoa
pole kwa wafiwa kwa kuondokewa na mpendwa wao, lakini sisi kama mamlaka na
taifa kwa ujumla tumempoteza mtu muhimu sana aliyekuwa mchapakazi, tutamkumbuka
sana marehemu,” alisema Bw. Hanga.
Marehemu ambaye ameacha mume Bw. Alex Temba
na watoto wawili, Faith (9) na Harieth (4) alihamishiwa TAA tarehe
01/04/2016 akitokea Halmashauri ya Manispaa ya mji wa Songea alipokuwa akifanya
kazi kama mwanasheria kuanzia mwaka 2012.
 |
Bw. Alex Temba (wa pili kushoto), mume wa marehemu aliyekuwa Mwanasheria wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania
(TAA) kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bi.
Delfine Mulogo akiwa na binti yake Faith Temba (mwenye gauni jeupe) wakitoa
heshima za mwisho katika kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Augustine
lililopo Mbezi Temboni kabla ya kusafirishwa kwa mazishi katika Kijiji cha Uru
Kishumundu mkoani Kilimanjaro.
|
Naye Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria
Tanzania (TLS), Bw. Stephen Msechu alisema marehemu alikuwa mwanachama tangu
alipoapishwa kuwa Wakili mwaka 2012 na kupewa namba ya uanachama 3361 na
amekuwa akishirikiana nao katika shughuli mbalimbali kwa uadilifu mkubwa.
Hata hivyo, Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia
ya Mtakatifu Augustine lililopo Mbezi Temboni, Padri Fidelis Mfaranyembo
aliwataka waombolezaji waliofika kuuaga mwili wa marehemu Delfine kujiandaa wakati wote kwa kuwa hawajui siku wala saa watakayotwaliwa.
 |
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA), Bw. Lawrence Thobias akitoa heshima zake kwa mwili wa aliyekuwa
Mwanasheria Kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA), Bi. Delfine Mulogo aliyefariki Desemba 25. Marehemu atazikwa Kijiji cha
Uru Kishumundu mkoani Kilimanjaro. |
Padri Mfaranyembo alisema pia waombolezaji
wahakikishe wanakuwa watu wa sala wakati wote ili kumuombea marehemu aweze
kupokelewa na aingie katika ufalme wa mbinguni, kwani ufalme huo upo kwa kuwa
kunamaisha baada ya kifo.
“Kuna mwanafalsafa mmoja wa zamani, Plato
alitafakari sana kuwa mwanadamu akifa
anakwenda wapi? na akaona kila mwanadamu anabeba roho ya muumbaji na hivyo unapokufa roho inarudi kwa yule
aliyeiumba, "alisema na kuongeza:
 |
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Bi. Agnes
Kijazi akimpa pole Bw. Alex Temba kufuatia kifo cha Mkewe Bi. Delfine Mulogo
aliyekuwa Mwanasheria kwenye Kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Julius Nyerere (JNIA) aliyefariki Desemba 25 na atazikwa Kijiji cha Uru
Kishumundu mkoani Kilimanjaro. |
" Plato anatufundisha ya kwamba mwisho wa maisha yake hapa duniani
Mwanadamu anarudi kwa Mungu wake kulingana na namna alivyokuwa akiishi na
wengine hapa duniani,” alisema Padri Mfaranyembo.
Pia amemtaka mume wa marehemu Bw. Temba
asifadhaike kwa kuondokewa na mkewe, bali ajikabidhi kwa Mungu kwa kumuomba
hakika atamsaidia kwa kumtia nguvu na kumpa uwezo wa kuendelea kuwahudumia
watoto wake kwa kadri ya uweza wake Mungu.
 |
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA) wakijumuika na waombolezaji wengine katika misa ya kumwombea
marehemu Bi. Delfine Mulogo aliyekuwa Mwanasheria kwenye Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
|
Marehemu alipata elimu ya msingi katika shule
ya Oysterbay (1991), baadaye sekondari ya St. Mathew (1998), na baadaye elimu
ya Kidato cha Tano na Sita katika shule ya Wasichana ya Kibosho (2004), na
mwaka 2008 alihitimu Shahada ya Kwanza ya Sheria katika Chuo Kikuu cha
Tumaini.
 |
Mweka Hazina wa Klabu ya Uchukuzi, Bw.
Benjamin Bikulamchi (kulia), akimkabidhi rambirambi aliyewahi kuwa
Katibu wa Klabu hiyo, Bw. Alex Temba aliyefiwa na mkewe Bi. Delfine Mulogo
aliyekuwa Mwanasheria Kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius
Nyerere (JNIA).
|
 |
Viongozi wa Shirikisho la Michezo la Wizara
na Idara za Serikali (SHIMIWI), Bi. Itika Mwankenja na Bi. Joyce Benjamin
wakitoa rambirambi zao kwa Katibu Msaidizi wa shirikisho hilo Bw. Alex Temba
(kushoto) aliyefiwa na Mkewe Bi. Delfine Mulogo wakati wa misa ya kumwombea
marehemu iliyofanyika jana katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu
Augustine lililopo Mbezi Temboni.
|
Bwana Ametoa na Bwana Ametwaa Jina Lake Lihimidiwe. Amina.