Monday 23 October 2017

Real Madrid yaifukuza Barcelona kimya kimya

MADRID, Hispania

MABINGWA watetezi wa La Liga Real Madrid imefanya kweli baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Eibar na kupunguza tofauti ya pointi na vinara Barcelona, huku Karim Benzema akianzia benchi.

Marco Asensio aliing’arisha Real Madrid baada ya kufunga mabao mawili na kuiwezesha timu yake hiyo kuibuka na ushindi huo.

Kwa ushindi huo, Real Madrid sasa imepunguza tofauti ya pointi na Barcelona hadi kufikia tano katika mbio hizo za kusaka ubingwa.

Mshambuliaji huyo alilazimisha bao la kujifunga na kufunga la pili wakati Madrid ikipanda hadi katika nafasi ya pili ikifikisha pointi 20, moja nyuma ya Valencia na moja mbele ya Atletico Madrid, ambayo iliifunga Celta Vigo 1-0 ugenini.

Bao hilo pekee lililoipatia ushindi Atletico Madrid liliwekwa kimiani na Kevin Gameiro.

Barcelona wenyewe waliwafunga Malaga 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wao wa Nou Camp Jumamosi wakati Valencia ilipoisambaratisha Sevilla 4-0.

Paulo Oliveira aliijaza katika wavu wao krosi ya Asensio katika dakika ya 18, kabla mshambuliaji huyo hajawafungia wenyeji bao la pili dakika 10 baadae kufuatia mpira wa Isco.

Mchezaji aliyeingia akitokea benchi Marcelo aliongeza la tatu katika dakika 82.


Zinedine Zidane alifanya mabadiliko matano kutoka katika kikosi chake, ambacho kilitoka sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Tottenham Hotspur katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya Jumanne iliyopita.

No comments:

Post a Comment