Friday 7 October 2016

Neymar afunga Brazil ikiiadhibu Bolivia kwa mabao 5-0 mbio za kwenda Urusi 2018


Neymar wa Brazil (kulia) akichuana na mchezaji wa Bolivia, Yasmani Duk wakati wa mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia Urusi 2018 uliofanyika jana Natal, Brazil. Wenyeji walishinda mabao 5-0.

BRASILIA, Brazil
MCHEZAJI nyota Neymar alifunga bao moja na kutengeneza mengine mawili zaidi wakati Brazil ikiibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Bolivia katika mbio za Amerika ya Kusini za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018.

Neymar, ambaye ni nyota wa Barcelona alifunga bao la 49 katika mechi ya kimataifa ikiwa ni mara yake ya 73 kuichezea Brazil na kumzidi Zico katika ufungaji wa mabao mengi wa wakati wote. 

Akiwa bado na umri wa miaka 24 tu, Neymar anaweza kufikia rekodi ya Pele ya kufunga mabao 77 kutoka katika mechi 91 huku akiwa bado namechi kadhaa kabla ya kufikia 91.

Ushindi huo wa Brazil umeiacha timu hiyo ikiwa katika nafasi nzuri ya kutwaa nafasi ya kufuzu kwa fainali ya Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi. 

Timu hiyo sasa inashika nafasi ya pili katika msimamo ikiwa na pointi 18 baada ya kucheza mechi tisa. 

Pia huo ni ushindi wa tatu mfululizo kutoka katika mechi tatu kwa kocha Tite, aliyeteuliwa baada ya kutimuliwa kwa Dunga Juni. 

Mbali na Neymar, wachezaji wengine walioingarisha Brazil kwa mabao ni pamoja na Philippe Coutinho, Filipe Luis na  Gabriel Jesus na kuiwezesha timu hiyo kuwa mbele kwa mabao 4-0 hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.

Mchezaji mwenzake Coutinho katika Liverpool, Roberto Firmino alifanya matokeo kuwa mbele kwa 5-0 kwa bao la kichwa lililofungwa katika dakika ya 75.

Neymar aliifungia Brazil bao la kuongoza katika dakika ya 10 tu.  Brazil sasa itasafiri hadi Venezuela kucheza Jumanne dhidi ya timu hiyo ambayo haijashinda hata mchezo mmoja.

No comments:

Post a Comment