Wednesday 12 October 2016

Brazil yatua kileleni wakati Argentina ikichapwa nyumbani mbio za kusaka kufuzu Kombe la Dunia 2018



BRASILIA, Brazil
BRAZIL imetinga kileleni mwa msimamo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018 kwa Kanda ya Amerika ya Kusini, baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Venezuela wakati Argentina ikipokea kichapo nyumbani kutoka kwa Paraguay.

Mabao kutoka kwa chipukizi wa Manchester City, Gabriel Jesus na mchezaji wa Chelsea Willian yaliiwezesha timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Venezuela katika mchezo ulioingiliwa na kuzimika kwa taa na kuufanya Uwanja wa Metropolitano wa Estadio kuwa giza.

Ushindi huo ni wa nne mfululizo kwa Brazil katika kampeni hizo za kufuzu na kuwaacha mabingwa hao mara tano wa dunia kuongoza katika msimamo wakiwa na pointi 21 baada ya kushuka dimbani mara 10.

Ushindi huo pia ni ushahidi wa hivi karibuni kabisa kuwa Brazil chini ya kocha mpya Tite, aliyeichukua timu hiyo baada ya kutimuliwa kwa Dunga Juni baada ya timu hiyo kufanya vibaya katika michuano ya Copa America Centenario, iko vizuri.

Ni mara ya kwanza kwa Brazil kuongoza msimamo huo tangu kuanza kwa kamapeni za kufuzu, na timu inaonekana ikiendelea vizuri na inaelekea kuendeleza rekodi yake ya kutowahi kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia.

Hatahivyo, mtihani mkubwa kwa Brazil utakuwa mwezi ujao na hapo ndipo itadhihirisha kama makali yao sio ya muda wakati itakapokutana na wapinzani wao wazamani Argentina, ambao juzi walipokea kichapo cha bao 1-0 nyumbani kutoka kwa Paraguay huko Cordoba.

Bao lililotokana na shambulizi zuri la kushtukiza kutoka kwa mshambuliaji Derlis Gonzalez katika dakika ya 18 lilitosha kabisa kuipatia Paraguay pointi zote tatu wakati wenyeji kwa mara nyingine tena wakijaribu kuzoea kucheza bila nyota wao wanaomtegemea sana Lionel Messi.

Argentina imeambulia pointi mbili tu badala ya tisa zilizotakiwa katika mechi zake tatu zilizopita, ambazo zote walikipiga bila yakuwepo Messi.

Timu hiyo ya Argentina ilionekana kubadilika katika kipindi cha pili, huku Angel Di Maria akinusurika kufunga baada ya mpira wake wa adhabu kushindwa kutinga wavuni huku Gonzalo Higuain na Sergio Aguero nao wakikaribia kupata mabao.

Ushindi huo umeiacha Paraguay ikiwa pointi moja nyuma ya Argentina katika msimamo baada ya mechi 10. Argentina iko katika nafasi ya tano kimsimamo ikiwa na pointi 16, huku Paraguay ikiwa nyumabaada ya kujikusanyia pointi 15.

CHILE YASHINDA
Wakati huohuo, Chile, imeendelea kuwa nje ya nafasi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018 licha ya juzi kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Peru katika mchezo uliofanyika Santiago katika mchezo ambao wengi wanautambua kama "Clasico del Pacifico."

Chile,ambayo katika miaka miwili iliyopita ilitawala soka la Amerika ya Kusini kwa kushinda mara mbili mfululizo taji la Copa America, ilihitaji pointi tatu ili kurejea katika mstari baada ya kuanza vibaya kampeni zake hizo za kufuzu.

Kiungo wa Bayern Munich Atrudo Vidal aliipatia bao "La Roja" au `Wekundu kama inavyojulikana timu ya taifa ya Chile, na kuipatia matumaini ya kufanya vizuri kwa bao hilo la kuongoza la dakika ya 10 na kuifanya Chile kuwa mbele kwa bao 1-0.

Juhudi za Peru zilizaa matunda katika dakika ya 76 wakati Edison Flores alipofunga bao kwa shuti hafifi na kufanya matokeo kuwa 1-1.

Ilionekana kama Peru imefanikiwa kuondoka na pointi moja wakati muda ukuzidi kuyoyoma, lakini Vidal alipata nafasi katika eneo la penalti na kupiga shuti hafifu lililompita Pedro Gallese na kujaa wavuni.

Ushindi huo wa Chile umeiacha timu hiyo ikiwa ya saba katika msimamo kwa kuwa na pointi 14, mbili kutoka nafasi za kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia.

Mapema, vinara Uruguay walitoka sare ya mabao 2-2 na timu ya Colombia iliyopo katika nafasi ya nne.

No comments:

Post a Comment