Wednesday 26 October 2016

Mwenyekiti Riadha Zanzibar ajitosa kuwania ujumbe Kamati Olimpiki Tanzania (TOC)



Na Mwandishi Wetu
WAKATI wadau wa michezo Tanzania Bara wanasita kujitokeza kuchukua fomu za kuwania uongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Zanzibar kumekucha baada ya kiongozi mmoja wa michezo kukata utepe kwa kuchukua fomu.

Kiongozi huyo ni Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Zanzibar (ZAA), Abdulhakim Cosmas kuchukua fomu leo akitaka ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TOC.

Rais wa TOC, Gulam Rashid amesema leo kuwa, Cosmas anawania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TOC.

Akizungumzia mchakato mzima wa kuchukua fomu ulioanza jana Jumanne, Rashid alisema kuwa unaendelea taratibu na wadau wengi wa michezo wanafika katika ofisi ndogo za TOC Zanzibar na kuchungulia na kuondoka.

Watu bado wanasuasua kwani baadhi yao wanakuja na kuondoka, alisema Gulam katika mahojiano maalum leo Jumatano.

Kwa upande wa Tanzania Bara, hadi leo jioni saa 10:00 wakati ofisi za TOC zilizoko Mwanyamala jengo la Biashara Complex zikifungwa hakuna mdau yeyote wa michezo aliyejitokeza kuchukua fomu yeyote.

Nafasi zinazowaniwa ni pamoja na Rais, Makamu wa Rais, Katibu Mkuu, Katibu Mkuu Msaidizi, Mhazini Mkuu, Mhazini Msaidizi na wajumbe 10 wa Kamati ya Utendaji.

No comments:

Post a Comment